Habari Mseto

Njia ‘mboga’ ya mama mboga kumiliki nyumba za bei nafuu

January 11th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

SUALA tata la mpango wa makazi ya bei nafuu kwa Wakenya linazidi kuibua hisia ambapo hivi punde, wengi wanajiuliza kuhusu namna ya kupata nyumba hizo.

Ila kupata nyumba ya vyumba viwili vya malazi Kaunti ya Nakuru, itamhitaji mkodishwaji kulipa amana yaani ‘deposit’ ya angalau Sh315,000 na kodi ya Sh16,997 kila mwezi ili kumiliki nyumba hiyo hatimaye.

Haya ni kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawishaji wa Miji.

Tangazo hilo limewataka wanaonuia kununua nyumba hizi wazitembelee eneo la Bondeni mjini Nakuru ili kuzikagua sababu ziko tayari kuchukuliwa.

Nyumba hizo zenye vyumba viwili na vitatu vya malazi ni za gharama ya Sh3,150,000 na Sh4,250,000 mtawalia.

“Wanunuzi watahitajika kulipa rubuni ya asilimia 10 ili wahitimu mahitaji ya kupata nyumba hizi,” ilisema sehemu ya notisi ya wizara.

Notisi hiyo ikaendelea kusema: “Wanunuzi watapewa mkopo wa nyumba ili wamiliki makazi haya wakilipa Sh16,997 na Sh22,933 kwa nyumba ya vyumba viwili na vitatu vya malazi mtawalia.”

Viwango hivi vya kulipia makazi vinaenda kinyume na kauli ya Rais William Ruto aliyesema mahasla watalipa kodi ya Sh4,000 kila mwezi kumiliki nyumba hizi.

“Tunawapa mama mboga na wanabodaboda fursa ya kulipa kodi ya Sh4,000 kila mwezi ili kumiliki nyumba ya Sh400,000,” alisema Rais Ruto katika mahojiano na wanahabari mnamo Desemba 17, 2023.

Gavana wa Nakuru Susan Kihika alifurahia maendeleo haya akimsifu Rais.

“Ni vipi mtu yeyote anaweza kupinga hili? Nakuru imefurahi na ahsante sana Rais,” alisema kwenye akaunti yake ya mtandao wa X.

Haya yanajiri huku serikali ikiruhusiwa iendelee kuwakata Wakenya ushuru wa ujenzi wa nyumba.

Uamuzi wa kesi dhidi ya mpango huu utatolewa Januari 26, 2024.

Mnamo Jumatano Rais Ruto alizindua ujenzi wa nyumba nafuu katika eneo la Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Alidai kwamba wapo matajiri wasiotaka afaulu kuwatimizia mahasla ahadi alizotoa.

Aliahidi kukabiliana na makateli kuwatimizia mahasla ahadi za nyumba nafuu na mpango wa afya kwa wote.