Makala

ULIMBWENDE: Njia rahisi za kuondoa weusi kwenye magoti na kisugudi cha mkono

March 26th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

NGOZI nyeusi katika magoti na nyuma ya mikono hutokana na mkusanyiko wa seli zilizokufa, lakini pia unapoweka presha kwenye magoti na nyuma ya mikono yako.

Kama ukiwa unaweka mikono kwenye meza ukiwa kazini, ule msuguano unafanya ngozi iwe nyeusi hasa kwenye kisugudi.

Hata hivyo, huna haja ya kuwa na hofu kwa sababu unaweza kutumia njia hizi za asili kuondoa weusi huo:

Juisi ya Mshubiri au kwa lugha ya kitaalamu Aloe Vera 

Juisi ya Aloe Vera inasaidia kuondoa weusi. Unachotakiwa kufanya ni kupaka juisi hiyo kwenye sehemu yenye weusi na uache kwa nusu saa kisha unawe mikono na upake moisturiser. Rudia kufanya hivi mara angalau mbili kila siku.

Binzari, manjano, asali na maziwa

Changanya vyote hivi ambapo matokeo ni mchanganyiko mzito. Paka kwenye magoti na kwenye mikono yako palipo na weusi.

Kaa nao kwa nusu saa. Nawa na paka moisturiser. Rudia kufanya hivi kila siku kwa wiki kati ya 3-4. Bila shaka utapata matokeo mazuri.

Ndimu

Chukua pamba na uitumie kupaka juisi ya ndimu katika sehemu zenye weusi. Au unaweza kuikata tu ndimu na kuipaka kwenye sehemu unapotaka kuondoa uweusi. Kaa nayo kwa muda wa saa moja kisha nawa. Rudia hivi kila siku hadi weusi utakapopotea.

Mafuta ya mizeituni na sukari

Changanya vizuri, hii itakuwa kama scrub kwa ajili ya magoti na mikono.

Paka katika hizo sehemu zenye weusi kisha kuwa kama unamasaji polepole. Nawa kwa maji ya fufutende kisha paka moisturiser.