Michezo

Njogu ateuliwa kuinoa Thika United

May 9th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Thika United imemteua John Njogu kama kocha mkuu wa timu hiyo ili kuchua nafasi ya Nicholas Muyoti aliyejiuzulu wiki nne zilizopita.

Njogu awali alikuwa kocha wa Klabu ya Kiambu All Stars, Ruiru All Stars na kikosi cha sok cha Chuo Kikuu cha Mlima Kenya bewa la Thika

Kocha huyo chipukizi anatarajiwa ataongoza timu hiyo katika pambono dhidi ya klabu ya SoNy Sugar siku ya Jumapili katika uwanja wa Manispaa ya Thika.

Njogu atasaidiwa na Haji Bilali ambaye mchango wake klabuni kama mchezaji miaka ya nyuma bado inatambulika hadi leo.

Kocha Muyoti aliagana na Thika United inayodhaminiwa na kampuni ya Brookside Tarehe 1 mwezi Mei kufuatia misururu ya matokeo mabaya

Njogu ambaye aliandaa mazoezi mepesi na timu yake mpya siku ya Jumanne alitangaza uteuzi wake kupitia akaunti yake ya Facebook.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu na marafiki zangu ambao wamenisaidia kuafikia ndoto yangu. Nimeshiriki mazoezi yangu ya kwanza kama kocha wa klabu ya Thika United,” ikasema chapisho lake.

Kuteuliwa kwa kocha huyo hata hivyo kumewashangaza mashabiki wa soka waliotarajia timu hiyo kuteua mojawapo wa makocha maarufu na mwenye uzoefu.

Katika kipindi kisichozidi mwaka moja, Thika United wameweza kubadilisha makocha mara tatu. Alihudumu aliyekuwa naibu kocha wa Harambee Stars James Nandwa, akaja Nicholas Muyoti na sasa Njogu.

Makocha wengine wa zamani wa klabu hiyo ni Kocha wa vijana wasiozidi umri wa miaka 23 John Kamau na kocha mtajika Juma Abdalla.

Thika United wanakalia nafasi ya 16 ambayo ni eneo hatari la kushushwa ngazi kwenye msimamo wa jedwali la ligi baada ya kuvuna alama 12.