Dondoo

Njoo umchukue mtoto wako, lofa amzushia polo

June 16th, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

KIPSITET, KERICHO

Mlofa wa hapa aliwakosesha walevi raha mangweni alipozusha akimlaumu barobaro mmoja kwa kumuachia jukumu la kulea mtoto wake.

Inaarifiwa kuwa mlofa alipata jiko miezi michache iliyopita.

“Alimuoa mwanadada aliyekuwa na mtoto mchanga aliyezaa na jamaa mwingine lakini hiyo haikumzuia mlofa kumpenda sana na kumfanya mkewe,” alisema mdokezi.

Juzi, mlofa alifika mangweni, akaitisha dozi na kufurahia akiwa kimya huku akifuatilia gumzo za wenzake kwa ukaribu bila kushiriki.

Stimu za dozi zilipompanda, jamaa alinyanyuka na kumsuta mwenzake vikali.

“Wengi wanajua wewe ndiye baba ya mtoto wa mke wangu! Unaponda raha kwa dozi ukiwa umeniachia kazi ya ulezi. Kuja umchukue mtoto wako,” mlofa alifoka akimnyoshea kidole barobaro huyo.

Makalameni wengine walimrushia mlofa cheche za maneno wakimlaumu kwa kuwaharibia starehe zao.

“Nani alikuambia umuoe kipusa mwenye mtoto huku vipusa wanaotamani ndoa wakiwa wengi sana? Ungeomba msaada wa kutongozia kipusa ambaye hajazaa. Hata sikuwahi kushiriki mahaba na mkeo,” barobaro aliteta kwa uchungu mno.

Hasira zilimpanda mlofa hata zaidi na akamkaribia kijana na kumkaripia.

“Badala ya kunishukuru kwa kukusaidia kwa ulezi wa binti unanisuta hivi? Lazima unakaa pembeni ukitegea msichana awe mkubwa ndipo ufike umchukue umuoze ili upewe mahari. Sitakubali hayo kamwe. Wajibika kwa mwanao kuanzia leo hii,” jamaa alilia.

Barobaro aliangua kicheko cha dharau na kupiga dozi naye mlofa akamsukuma hadi akaanguka chini.

Kilichofuata kikawa ni teke na mangumi hadi wakatenganishwa na kufukuzwa kwa mama pima.