Habari Mseto

Njoroge kuendelea kuwa gavana wa Benki Kuu ya Kenya

June 6th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amemteua Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt Patrick Njoroge, kuhudumu kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Wakati huo huo, Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich alitangaza Bw James Githii Mburu ndiye Kamishna mpya wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) kuchukua mahali pa Bw John Njiraini.

Bw Mburu atahudumu katika wadhifa huo kwa miaka mitatu.

Kwenye tangazo lililotolewa katika gazeti rasmi la serikali jana, Dkt Njoroge ataanza kuhudumu rasmi mnamo Juni 11. Muda wake wa kuhudumu ulitarajiwa kuisha mnamo Juni 19.

Rais vile vile aliwateua upya Bw Jairus Nyaoga na Bi Sheila M’Mbijiwe kama mwenyekiti wa bodi na Naibu Gavana wa Benki mtawalia. Wawili hao pia watahudumu kwa kipindi cha miaka minne.

Uteuzi huo unajiri huku Kenya ikitarajiwa kuanza kutumia pesa mpya kuanzia mwezi Oktoba. Gavana huyo alitangaza kuzinduliwa kwa fedha hizo mnamo Juni 1, kwenye sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka.

Wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi walikuwa wametabiri uteuzi wake mpya ili kuisaidia Serikali Kuu kuendesha utaratibu wa kuanzisha matumizi ya pesa hizo.?Dkt Njoroge alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Prof Njuguna Ndung’u mnamo 2015. Na kufuatia uteuzi huo, atahudumu hadi mwaka 2023.

Uteuzi wake pia unatarajiwa kuisaidia serikali kuimarisha mkakati wa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kupitia Benki Kuu.

Wachanganuzi wanasifia juhudi zake za kuiwezesha shilingi kuwa thabiti ikilinganishwa na pesa za nchi nyingine, ambazo udhabiti wake umekuwa ukiyumba.

“Amejaribu kudumisha uthabiti wa shilingi, hali ambayo imechangia sana katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” asema Tony Watima, ambaye ni mwanauchumi.

Dkt Njoroge, ambaye alisomea masuala ya uchumi nchini Amerika alihudumu kama mshauri wa kiuchumi katika Shirika la Fedha Duniani (IMF) kabla ya kuteuliwa gavana.