Nkana FC anayochezea Mkenya Abuya yaendea muujiza dhidi ya Pyramids soka ya CAF

Nkana FC anayochezea Mkenya Abuya yaendea muujiza dhidi ya Pyramids soka ya CAF

Na GEOFFREY ANENE

NKANA inayoajiri Mkenya Duke Abuya inatarajiwa kupata mtihani mkali itakapofungua mechi zake za makundi za Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederations Cup) dhidi ya wenyeji Pyramids jijini Cairo, Misri, Jumatano jioni.

Mabingwa hao wa Zambia wako katika kundi ngumu la D pamoja na Pyramids (Misri), Raja Casablanca (Morocco) na Namungo (Tanzania).

Nkana wamekuwa na msimu mbaya nyumbani. Wako katika mduara hatari wa kutemwa kwenye Ligi Kuu baada ya kuokota alama 20 kutokana na michuano 17 wamesakata.

Wamepoteza mechi tatu mfululizo ligini humo, huku ushindi wao wa mwisho ukiwa dhidi ya TS Casablanca 2-0 Februari 12 nchini Zambia kwenye dimba hili. Waliingia mechi za makundi za Confederations Cup baada ya kulemea TS Casablanca kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kupoteza mechi ya marudiano 2-1 nchini Morocco.

Nkana watatumai kupata matokeo mazuri dhidi ya Pyramids ambayo inashikilia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Misri. Pyramids imeshinda mechi mbili zilizopita ligini humo na haijapoteza sita mfululizo katika mashindano yote. Ilibandua Racing d’Abidjan ya Ivory Coast katika raundi iliyopita kwa jumla ya mabao 4-0.

Nkana, ambayo inanolewa na kocha Kevin Kaindu, pia imekuwa na rekodi duni dhidi ya timu kutoka Kaskazini mwa Afrika.

“Mambo yamekuwa magumu kila tunapokutana na wapinzani kutoka Kaskazini mwa Afrika, lakini nadhani hatujafika hapa kimiujiza,” alieleza tovuti ya Nkana.

“Tatizo letu kubwa limekuwa katika idara ya makipa na tutajaribu kutafuta suluhisho itakayodumu muda mrefu. Matumaini yangu ni kuwa kipa tutakayetumia dhidi ya Pyramids atafanya kazi nzuri,” aliongeza Kaindu.

Raja Casablanca inaongoza Ligi Kuu ya Morocco nayo Namungo ni ya tisa kwenye Ligi Kuu Bara inayojumuisha klabu 18.

You can share this post!

SAUTI YA MKEREKETWA: Ada inayotozwa na KICD ili kuidhinisha...

FC Porto yaangusha miamba Juventus kwenye soka ya UEFA...