Nketiah aokotea Arsenal pointi moja dhidi ya Fulham katika EPL

Nketiah aokotea Arsenal pointi moja dhidi ya Fulham katika EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Scott Parker wa Fulham amesema “haelewi” jinsi ambavyo bao la dakika ya mwisho kutoka kwa fowadi Eddie Nketiah wa Arsenal lilivyokubaliwa na refa katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na vikosi hivyo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili uwanjani Emirates.

Kwa mujibu wa Parker, Nketiah alifunga goli hilo wakati ambao beki Rob Holding wa Arsenal alikuwa ameotea, kando ya kipa Alphonse Areola aliyekuwa awali amemnyima Dani Ceballos fursa nyingine ya kucheka na nyavu.

Hata hivyo, kwa kuwa Holding hakugusa mpira, ilifasiriwa na refa kwamba hakuathiri mchezo wala mkondo wa mpira uliojazwa kimiani na Nketiah sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Bao hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Fulham waliowekwa uongozini na Josh Maja kunako dakika ya 59 kupitia penalti iliyosababishwa na beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes aliyemchezea vibaya Mario Lemina ndani ya kijisanduku. Alama tatu kwa Fulham zingaliweka hai matumaini yao finyu ya kutoshushwa ngazi kwenye kampeni za EPL mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, kikosi hicho kwa sasa kinasalia katika nafasi ya 18 kwa alama 27, nne pekee kuliko nambari 19 West Bromwich Albion. Sheffield United wanaovuta mkia kwa pointi 14 kutokana na mechi 32 zilizopita, tayari wameteremshwa ngazi kutoka EPL hadi Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) msimu ujao wa 2021-22.

“Lilikuwa bao la uchungu sana, ambalo huenda limezamisha kabisa matumaini yetu ya kusalia kwenye kampeni za EPL msimu ujao. Hata hivyo, tutaendelea kupigana hadi mchuano wa mwisho,” akasema Parker.

Sasa ni pengo la alama sita ndilo linatamalaki kati ya Fulham na Burnley waliosalia katika nafasi ya 17 baada ya kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Manchester United uwanjani Old Trafford.

Mbali na Nketiah na Ceballos aliyeshuhudia bao lake la kipindi cha kwanza likifutiliwa mbali kwa madai kwamba kiungo Bukayo Saka alikuwa ameotea, wanasoka wengine wa Arsenal waliojituma maradufu dhidi ya Fulham ni fowadi chipukizi Gabriel Martinelli na Emile Smith Rowe.

Nusura fowadi Nicolas Pepe naye afungie Arsenal bao katika kipindi cha pili ila juhudi zake zikazimwa na kipa Areola.

Arsenal waliosalia katika nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 46, sasa wanajiandaa kuvaana na Everton mnamo Aprili 23 April, wiki moja kabla ya Fulham kuwaendea Chelsea uwanjani Stamford Bridge.

MATOKEO YA EPL (Aprili 18, 2021):

Arsenal 1-1 Fulham

Man-United 3-1 Burnley

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Biashara ya mitandaoni yawaletea Wakenya fursa mpya ya...

TAHARIRI: Unyama wa polisi si dawa ya corona