Habari MsetoSiasa

NLC na KR lawamani kukosa kufidia wakazi Sh5.8b

July 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKUU wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na Shirika la Reli Nchini (KR) Jumanne walielekezewa lawama na wabunge kuhusiana na suala la kutolipwa kwa ridhaa kwa watu ambao ardhi zao zilitwaliwa kutoa nafasi kwa ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya kisasa SGR.

Hii ni baada ya kubainika kuwa jumla ya wakazi 200 wa eneo la Ngoroi, kaunti ndogo ya Ongata Rongai, Kajiado Kaskazini hawajalipwa jumla ya Sh5.8 bilioni kama fidia kwa ardhi iliyotwaliwa kwa ujenzi wa reli hiyo kutoka Nairobi hadi Naivasha.

Wabunge walimlaumu Kaimu Afisa Mtendaji wa NLC Bi Kabale Beche kwa kushikilia pesa hizo za ridhaa kwa zaidi ya miaka miwili licha ya nyumba za wahusika kubomolewa.

“Inasikitisha kwamba ujenzi wa reli hii unaelekea kukamilika ili izinduliwe na Rais Uhuru Kenyatta mwezi ujao wa Agosti ilhali jumla ya watu 200 mbili ambao ardhi ya ilitwaliwa hawa, Isitoshe, baadhi yao walipata hasara kubwa baada ya mali yao kuharibiwa nyumba zao zilipoteketezwa na maafisa wa polisi waliokodiwa na Shirika la Reli Nchini (KR),” akasema Mwenyekiti wa Kamati hiyo David Pkosing.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KR Philip Mainga alielekezewa lawama kufuatia baada ya shirika lake kubomoa nyumba za wakazi wa Ngoroi bila kuwapa notisi kisheria.

Jaribio lake la kujitetea kwamba shirika lake lilitoa ilani kwa wakazi kupitia mikutano ya baraza iliwakasirisha zaidi wabunge waliosema kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume cha sheria.

“Kisheria, illani hutolewa kwa maandishi kwa wahusika. Watu hupewa muda fulani, tusema mwezi mmoja au miezi miwili kutoa mali ya kabla ya hatua zozote kuchukuliwa.

“Kwa hivyo, hii ina maana kuwa hatua ya shirika la reli kubomoa nyumba za wakazi ilikuwa ukatili ambao haufai kutendewa Mkenya yeyote katika enzi hii,” akasema Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama.

Suala hilo la kutolipwa ridhaa kwa wakazi wa Ongata Rongai lilikuwa limeibuliwa na Mbunge wa Kajiado Kaskazini Joseph Manje ambaye alitaka kufahamishwa kuhusu ni lini watu hao watalipwa ridhaa.

Baada ya wabunge kutuliwa cheche za maneno, Bi Beche aliwahakikisha kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi huu, wale wote ambao hawajalipwa ridhaa watapokezwa pesa zao.

“Ningependa kuwahakikishia kamati hii, raia wahusika wa eneo la Ongata Rongai na Wakenya kwa jumla kwamba Sh5.8 bilioni zilisalia zitakuwa zimelipwa,” akasema huku akiongeza kuwa kuchelewa huko kulisababishwa na uchunguzi uliokuwa ukiendeshwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu watu fulani waliowasilisha madai bandia ya Sh130 milioni.