Habari Mseto

NLC yashindwa kuelezea ziliko Sh2 bilioni

March 14th, 2018 1 min read

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi Dkt Muhammad Swazuri. Picha/ Maktaba

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) Jumanne ilishindwa kuwashawishi wabunge iwapo Sh2.1 bilioni ilizolipa kama ridhaa kwa ardhi zilizotwaliwa na serikali kwa ujenzi wa miradi ya miundomsingi ziliwakilisha thamani halisi ya vipande husika vya ardhi.

Miradi hiyo ni kama vile, ujenzi wa bandari ya Lamu, barabara za Outering (Nairobi), Dongo Kundu (Mombasa) kati ya mingine.

Wakihojiwa na wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) kuhusu suala hilo, maafisa wa tume hiyo wakiongozwa na mwenyekiti Mohammed Swazuri walikiri kwamba hawakuwasilisha stakabadhi za malipo kwa mhasibu mkuu wa fedha za serikali kwa wakati.

“Ni kweli kwamba tulichelewa kuwasilisha maelezo muhimu kama vile nambari za ploti, ekari za ardhi husika, ripoti ya utathmini wa ardhi na stakabadhi za benki kwa maafisa kutoka afisi ya mkaguzi wa hesabu kwa wakati uliowekwa.

Lakini hii haimaanishi kuwa tulipania kuficha ukweli wowote,” akasema Bi Salome Munubi, ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Ubainishaji Thamani ya Ardhi katika NLC.

Lakini kulingana na ripoti ya Mkaguzi wa Pesa za Serikali ya mwaka wa kifedha za 2015/2016 tume hiyo ilifeli kutoa stakabadhi ya kuthibitisha namna Sh2.1 bilioni kama ridhaa kwa niaba ya asasi mbalimbali za serikali.

“NLC ilifeli kuwasilisha ripoti ya ukadiriaji thamani ya ardhi na maelezo mengine ambazo zilihitajika wakati wa ukaguzi wa jinsi pesa hizo za ridhaa zilivyotumika,” ikasema ripoti hiyo iliyolewa na Bw Edward Ouko.

Hata hivyo, NLC iliwaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kwamba wamekwisha wasilisha maelezo yaliyohitajika na afisi ya Bw Ouko wiki jana, jibu ambalo halikuwafurahisha wabunge hao.