NLC yataka maskwota wa tangu ukoloni sasa wapewe makao

NLC yataka maskwota wa tangu ukoloni sasa wapewe makao

Tom Matoke na Onyango K’Onyango

TUME ya Kitaifa kuhusu Ardhi (NLC) imeiomba Wizara ya Ardhi kuwatafutia makao zaidi ya watu 500 ambao wamekuwa maskwota tangu enzi ya ukoloni katika Kaunti ya Nandi.

Kwa miaka mingi, watu hao wamekuwa wakiishi kama maskwota na katika umaskini mkubwa katika shamba la mikonge la Chemelil.Hata hivyo, wamepata matumaini mapya baada ya tume hiyo kuagiza wapatiwe makao katika ardhi ya ekari 1, 440 kwenye shamba hilo.

Ardhi hiyo ni sehemu ya vipande sita vya ardhi vilivyo kwenye shamba hilo kubwa. Nambari ya usajili ya kipande cha ardhi ambako wameagizwa kupewa makao ni LR 7057.

Tume pia imeiagiza serikali ya Kaunti ya Nandi kuhakikisha kuna nafasi ya kujengea taasisi muhimu kama shule na masoko wakati itakapokuwa ikiendesha zoezi la ugavi wa ardhi hiyo.

Kwenye barua aliyoandikiwa Waziri wa Ardhi, Farida Karoney mnamo Februari 9, tume ilisema imeidhinisha maskwota hao kupewa makazi baada ya kuandaa kikao kuangazia suala hilo.

Barua hiyo iliandikiwa waziri na Kamishna Reginald Okumu kwa niaba ya mwenyekiti wa tume, Bw Gershom Otachi.

 

You can share this post!

Huenda wandani wa Ruto Kisii wakamtoroka hivi karibuni

Waziri motoni kukodisha choo kwa Sh2.3m