Michezo

NMG yamtambua Larry Ngala kwa mchango wake katika spoti

February 19th, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWANAHABARI mkongwe Larry Ngala Jumanne aliadhimisha miaka 70 tangu kuzaliwa kwake, na miaka 45 ya kufanya kazi katika Shirika la Habari la Nation Media Group (NMG).

Afisa Mkuu Mtendaji wa NMG, Bw Stephen Gitagama aliongoza usimamizi wa NMG kummiminia sifa Bw Ngala ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kama mwandishi mahiri wa habari za michezo, hasa gofu.

Alimshukuru Bw Ngala kwa kufuatilia, kuhudhuria na kushiriki mashindano mbalimbali ya gofu, vitendo vilivyomjengea himaya kama mwanahabari wa kipekee wa mchezo wa gofu nchini.

Keki yenye umbo wa gofu iliyoandaliwa mwandishi maarufu wa spoti Bw Larry Ngala. Picha/ Evans Habil

“Huyu mzee amejitolea sana kutimiza wajibu wake. Kila mara baada ya kushiriki makala mbalimbali ya gofu siku nzima, yeye hutenga muda na kuandika kuhusu matokeo ya mashindano hayo gazetini. Shukran sana na kila la kheri,” akasema Bw Gitagama.

Akihutubu wakati wa sherehe hiyo, ambapo wafanyakazi wenzake waliungana naye kukata kesi, Bw Ngala alisema siri ya ufanisi wake ni mwito na kujitolea kufanya kazi kwa bidii bila kujali maslahi ya kibinafsi kama yale ya kifedha.

“Tangu nijiunge na kampuni hii mwaka wa 1974 bidii na kupenda kazi yangu ndizo zimekuwa msingi wa ufanisi wangu. Nawaomba nyie wanahabari mpende kazi yenu bila kuweka mbele maslahi ya kibinafsi.”