Habari

NMS yaahirisha kuhamisha kwa matatu katikati mwa jiji hadi Januari

December 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) sasa imetangaza kuwa imeahirisha kufunguliwa kwa vituo vipya vya magari ya uchukuzi wa abiria nje ya katikati mwa jiji hadi mapema mwezi Januari, 2021.

Kulingana na taarifa kutoka idara hiyo hiyo inatokana na kutokamilika kwa ujenzi unaoendelea katika vituo hivyo kufikia Jumatatu wiki jana kama ilivyopangwa.

Kituo cha Green Park karibu na bustani ya Uhuru Park ambayo ilipangiwa kutumiwa na matatu yanayohudumu kati ya katikati mwa jiji na mitaa ya Kawangware, Kibera na maeneo ya Ngong’ ni moja ya vituo ambavyo ujenzi wavyo haujakamilika.

Kituo hicho, ambacho kiko karibu na Railway Club, kina uwezo wa kutumika na matatu 250.

Kituo kingine kiko katika makutano ya barabara za Bunyala Road na Workshop Road na kitahudumia magari ya uchukuzi ambayo hutumia barabara kuu ya Mombasa Road.

Magari ya uchukuzi kutoka eneo la Mlima Kenya ambayo hutumia kituo cha Tea Room katika barabara ya Accra yatahamishwa hadi kituo kipya kilichoko katika makutano ya barabara za Desai Road na Park Road katika mtaa wa Ngara.

Ujenzi wa kituo hicho ungali unaendelea.

Mkurugenzi mkuu wa NMS Mohammed Badi alisema atahakikisha kuwa matatu yote yanaondolewa katikati mwa jiji ili kupunguza msongamano wa magari na visa kadhaa vya usumbufu na wizi.