Michezo

NOC-Kenya yatangaza maafisa wa kuongoza jopo la kukuza wanamichezo wa Kenya

March 22nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KAMATI ya Olimpiki ya Kenya (NOC-Kenya) imemteua Humphrey Kayange kuongoza jopo la watu watano litakalosaidia kamati yake kuu katika majukumu ya kiufundi na kutoa ushauri kuimarisha mradi wake kukuza wanamichezo.

Wanakamati wengine katika jopo hilo litakalotoa ushauri kuhusu usimamizi wa udhamini wa wanamichezo, kutafuta habari kuhusu mradi huu wa udhamini na kuutathmini, usimamizi wa ratiba za mazoezi na kutathmini maombi ya udhamini, ni makocha Musa Otieno (soka), Julius Kirwa (riadha), Rosemary Owino (tenisi) na Felix Ochieng’ (raga).

Jopo hili litashirikiana na makocha kutoka mashirikisho mbalimbali ya michezo nchini kuhakikisha mradi wa udhamini unahudumia wanamichezo wote na timu zinazopata udhamini kutoka na kupitia NOC-Kenya. Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Kayange pia ni mwakilishi wa wanamichezo kwenye kamati kuu ya NOC-Kenya.

Majuzi, NOC-Kenya ilitangaza kuwapa wanamichezo wanane udhamini wa Sh75,043 kila mmoja kila mwezi ili kuwaandaa kwa Olimpiki za mwaka 2020 zitakazofanyika jijini Tokyo nchini Japan.

Wanamichezo hao ni Mercy Joseph (badminton), Carlos Ochieng’ (judo), Webster Lukose (unyanyuaji uzani), Gulraaj Sehmi (ulengaji shabaha), Emmanuel Korir (riadha), Brian Mutua (tenisi ya meza), Mathayo Mahabila (miereka kitengo cha freestyle) na Danilo Rosafio (uogeleaji).

Udhamini

Jopo la Kayange lilianza mikutano yake Ijumaa asubuhi na makocha wa wanamichezo waliopata udhamini ili kuhakikisha kuna usimamizi mzuri na kutathminiwa kwa mipango yao

“NOC-Kenya itatangaza udhamini zaidi hivi karibuni kwa wanamichezo na timu,” Katibu wa NOC-Kenya, Francis Mutuku amesema Ijumaa.

Kupitia jopo la Kayange, NOC-Kenya imesema itaanza kuzungumza na washauri kutoka fani mbalimbali kusaidia wanamichezo hao na timu.

Jopo hilo, Mutuku anasema, itafanya kazi na mashirika mbalimbali na taasisi zinazoweza kusaidia NOC-Kenya kupata mazingira bora ya wanamichezo hao kufanyia mazoezi.

Kwa mujibu wa Mutuku, NOC-Kenya inapanga kuwa na eneo maalum ya kukuza talanta. Kamati hiyo pia inalenga kuhakikisha wanamichezo wanapata mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za kisayansi katika fani zote nchini Kenya.