Makala

NORAH OWADE: Mpodoaji wa kisasa asaka makuu katika uigizaji

December 22nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa daktari sasa anapania kuibuka kati ya wanamaigizo mahiri Afrika kama Jackie Appiah ambaye hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood).

Msanii huyo ambaye ni mzawa wa Canada anaorodheshwa kati ya waigizaji waliobobea nchini Ghana.

Norah Owade anasema alivutiwa na uigizaji akiwa darasa nane aliposhawishiwa na mwalimu mmoja shuleni humo kwamba alionekana mwenye mvuto mzuri kama mwanamaigizo.

Kando na hayo binti huyu anatarajia kufuzu kwa shahada ya diploma katika masuala ya hoteli za kifahari kwenye chuo cha Kiriri Women University. Kando na uigizaji kipusa huyu amezamia zaidi kwenye taaluma ya msanii mpodoaji (makeup artist).

”Kusema ukweli bila kujigamba nimebobea zaidi kama mpodoaji ambapo huwapodoa wasanii wenzangu wa kila aina wakiwamo wanamuziki na waigizaji bila kusahau wateja wa kawaida,” anasema kipusa huyo na kuongeza kuwa ni taaluma anayopania kuitumia kama kitenga uchumi maishani mwake.

Anadokeza kwamba ametwikwa jukumu la kuwa mwelekezi katika filamu kadhaa pia anajivunia kushiriki filamu mbili kama mhusika mkuu.

Katika utangulizi wake mwaka 2016, alijiunga na kundi la King sir ACE Production aliposhiriki filamu iliyofahamika kama ‘Roll the film.’ Chini ya kundi la Bandilisha Production kando na kushiriki uigizaji ndiye mpodoaji (Makeup Artist).

Pia kwenye kundi hilo ameshiriki filamu kwa jina ‘Stuck in the middle,’ pia wanaandaa filamu inayoitwa ‘My way on the Highway.’

Kando na waigizaji demu huyu pia hupata ajira kuwapodoa wana harusi, wanamuziki na video vixen wakati wa video shuti.

Owade anasema anatamani sana kufanya kazi na wasanii wa Bongo Muvi kama Jackline Wolper na Wema Sepetu kati ya wengine.

Kwa waigizaji wa Nollywood anasema kando na Jackie Appiah pia angependa sana kushirikiana na Ini Edo ambaye amefanikiwa kushiriki zaidi ya filamu 100 tangu 2000 alipojiunga na sekta ya uigizaji. Edo anajivunia kuteuliwa kuwa jaji mwaka 2013 kwenye mashindano ya urembo ya miss Black Afrika UK Pageant.

Anashauri wasichana wenzeka wajitunze wala wasiwe wepesi wa kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na maprodusa wao ili wapate ajira.

”Kwa wanadada ambao hupenda mahusiano sapuli hiyo huwa wanashusha hadhi ya mwanamke katika tasnia ya burudani kwa ujumla,” alisema.

Kadhalika anawaambia wenzeka wafanye utafiti pia watumie mtandao wa youtube kujifunza zaidi kuhusu masuala ya maigizo pia jinsi ya kuwapondoa wateja wao vizuri.

Kama ilivyo desturi kwa taaluma zingine, uigizaji na upodoaji zina changamoto zake. Kisura huyu anasema kuwa kwa upodoaji nyakati zingine humwagiwa matusi ya kila aina na wateja wao wakiwalaumu kwa kazi mbaya.

”Kando na hilo pia wateja wengine huwaponda baada ya kuwapodoa na kuathiriwa na kemikali za vipodozi,” alisema na kuongeza kuwa suala hilo mara nyingi hufanya wateja wengine kusepa.

Anatoa mwito kwa serikali ianzishe mikakati mwafaka itakayowapa mwanya mzuri waigizaji chipukizi nchini kukuza talanta zao.