Habari MsetoSiasa

Noti nzee za thamani ya Sh7.3 bilioni hazikurejeshwa – Benki Kuu

October 2nd, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Patrick Njoroge Jumatano alitangaza kwamba, Wakenya hawakurejesha noti za zamani za Sh1,000 za thamani ya Sh7.3 bilioni ambazo matumizi yake yalipigwa marufuku nchini.

Hii ni baada ya makataa ya kuwasilisha noti hizo kukamilika mnamo Jumatatu. Gavana huyo alikuwa ametangaza kuzipiga marufuku mnamo Juni 1, 2019 wakati wa sherehe za madaraka katika Kaunti ya Narok.

Akitoa taarifa ya kina kuhusu mchakato mzima wa ubadilishanaji wa fedha hizo, Dkt Njoroge alisema CBK ililenga kupata noti za zamani za Sh1,000 zenye thamani ya Sh217 bilioni lakini ikafanikiwa kupata Sh209 bilioni kufikia Septemba 30.

“Ningependa kuwatangazia Wakenya kwamba, hadi kufikia mwisho wa mwezi uliopita, idadi ya noti mpya ambazo zilikuwa zimerudishwa ni 209,661,000. Thamani yao ni Sh209 bilioni kati ya Sh217 bilioni tulizotarajia zingerejeshwa. Ingawa hii ni asilimia 83.2 na inaonyesha kwamba tulifanikiwa pakubwa, hatujui zilizoko Sh7.3 bilioni,” akasema Dkt Njoroge katika afisi za CBK jijini Nairobi.

Mwanauchumi huyo alisema kwamba, Wakenya walibadilisha noti kwa wingi zaidi Agosti na akasema fedha ambazo hazikurejeshwa sasa ni karatasi, akishikilia hakuna hasara serikali imepata katika kuchapisha noti mpya.

Aidha, alifichua kwamba akaunti 3,172 za watu binafsi zilitambuliwa kama zilizoshukiwa kuwa na hila kwenye ubadilishanaji wa noti, akisema maafisa kutoka idara ya upelelezi(DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi(EACC) wanaendelea kuchunguza akaunti hizo kisha kupendekeza mashtaka dhidi ya washukiwa.

“Tunashuku wenye akaunti hizo kutokana na kiasi cha fedha walizowasilisha na uchunguzi unaendelea dhidi yao. Tumewapa maafisa wa DCI na EACC habari muhimu kuhusu watu hawa na ni jukumu lao kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao. Vilevile kuna akaunti nyingine 15 ambazo maafisa wetu na idara husika wanaendelea kuzichunguza kwa undani,” akaongeza.

Dkt Njoroge pia alisema idadi ya noti mpya zinazotumika kwa sasa ni za thamani ya Sh149 bilioni.