Siasa

Notisi yadunda kutaka kumng’atua naibu gavana Kisii

February 13th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI 

BAADHI ya madiwani katika Bunge la Kaunti ya Kisii wametoa notisi ya mswada unaolenga kumng’atua mamlakani Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda.

Notisi hiyo ilitolewa na diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha mnamo Jumanne wakati bunge hilo lilirejelea vikao vyake baada ya likizo ndefu.

“Ningependa kutoa notisi ya mswada unaolenga kumng’atua mamlakani Naibu Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda. Kunazo sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi yake na ukiukaji mkubwa wa Katiba ya nchi,” Bw Siocha alisema.

Mswada huo utaangaziwa tena baada ya siku saba.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisii Phillip Nyanumba aliwaomba waanzilishi wa mswada huo kuhakikisha utaratibu wote unaohitajika kisheria umefuatwa.

Kulingana na Bw Siocha, wenzake 51 wametia saini hoja hiyo isonge mbele.

Gavana wa Kisii Simba Arati hajakuwa na uhusiano mzuri na Dkt Monda.

Hii ni kwa sababu mahasimu wake kisiasa akiwemo mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini) ni marafiki wakubwa wa Dkt Monda.

Wengine ni Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi na baadhi ya madiwani (MCAs) ambao mnamo Novemba 25, 2023, walikutana na Dkt Monda katika boma lake lililoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache. Mkutano huo ulifanyika usiku.

Japo viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa mkutano wao ulikuwa wa kutathmini jinsi ya kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo, ilionekana wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakipanga njama kuhusu namna ya kumtenga Gavana Arati dhidi ya viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Mkutano huo kwa Dkt Monda ulijiri muda mfupi tu baada ya wanasiasa hao kuhudhuria hafla ya misa katika Kanisa Katoliki la Nyabururu ambapo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikuwa mgeni wa heshima.