Michezo

Novemba 6, Gor kuchuana na Everton ugani Goodison Park

September 13th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

Mabingwa watetezi wa kandanda humu nchini Gor Mahia watachuana na klabu ya Everton kutoka Uingereza Novemba 6, saa nne usiku.

Baada ya muda mrefu wa mashabiki kusubiri, hatimaye tarehe ya mechi hiyo ya kirafiki ilitolewa, ambapo Gor wanatarajiwa kujikakamua vilivyo.

Tayari tiketi za mechi hiyo itakayochezewa Uingereza zimeanza kuuzwa, za watu wazima zikiuzwa  kwa Sh650 na za watoto na watu waliozidi miaka 65 kwa Sh130.

Pesa zitakazokusanywa katika mechi hiyo zitaelekezwa katika hazina ya klabu ya Everton ambayo hutumika kusaidia jamii.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa klabu ya Kenya kuchuana na klabu inayoshiriki ligi ya EPL, katika mchanga wa bara Uropa.

Gor walipenya kuchuana na Everton baada ya kushinda tena taji la SportPesa Super Cup, wakati wa mechi zilizochezwa Nakuru kuanzia Juni 3 hadi 10, 2018

Mechi hizo zilihusisha timu nane kutoka ligi za Zanzibar ‘Jeshi la Kujenga Uchumi’, mabingwa wa Tanzania ‘Yanga FC’, Simba SC, Singida na za Kenya Gor Mahia, AFC Leopards, Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz.

Kwenye fainali, Gor ilicharaza Simba mabao 2-0 na kushinda taji tena, na ziara kuchuana na Everton katika uwanja wao wa nyumbani Goodison, UK.

Gor aidha inakuwa klabu ya kwanza ya ligi ya SportPesa kuchezea katika mchanga wa Uingereza nay a pili kutoka humu nchini, baada ya timu ya SportPesa AllStars ambayo ilichuana na Hull City katika uwanja wa KCOM Februari 27, 2017.

Timu ya AllStars ilijumuisha wachezaji kutoka vilabu tofauti vya ligi kuu ya SportPesa.