Habari Mseto

NTSA yaanzisha vituo vya mapumziko kwa madereva

August 20th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MAMLAKA ya Kitaifa ya usalama barabarani(NTSA) kwa ushirikiano na mashirika ya kibinafsi imeanzisha vituo 28 ambavyo vitakuwa vikitumika kama vituo vya mapumziko na matibabu  kwa madereva wa malori ya safari za masafa marefu.

Kupitia mpango ujulikanao kama  SWHAP (Swedish Workplace Hiv Aids Programme), NTSA inalenga  kupunguza idadi ya ajali zinazoshuhudiwa katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi-Malaba ambayo hutumiwa sana na madereva wa malori hayo.

Chini ya mpango wa uangalizi wa safari na mienendo wa madereva  maarufu kama CHECKMATE, zaidi ya madereva 1000 watahudumiwa  kila siku katika vituo ambavyo tayari vinafanya kazi  katika miji ya Maungu, Kericho, Garissa na Kisumu.

Akizungumza wakati wa kuzindua ushirikiano huo katika hoteli ya Panfric jijini Nairobi,  Mkurugenzi mkuu Francis Meja  alitaka mashirika nchini kuwasajili madereva wao chini ya mapango huo  ili kusaidia kuhakikisha usalama barabarani na kudhibiti mienendo ya madereva.

“Ninayaomba mashirika kuwasajili madereva wa masafa marefu katika mpango huu kwa kuwa tutafungua vituo 20 zaidi kando na hivi vinane ambavyo tunafurahia kusema  vimesaidia pakubwa kushusha idadi ya ajali kati ya Nairobi, Mombasa na mji wa mpakani wa malaba,” akasema Meja.

Aidha Bw Meja aliwaomba wadau katika sekta ya matatu i kukumbatia majadiliano kabla ya kushiriki mgomo unaotarajiwa wiki hii kufuatia ongezeko la bei ya mafuta huku wakitishia kuongeza nauli kwa wasafiri.

Mkurugenzi wa Shirika la kutoa ushauri kuhusu usalama barabarani(PRSC) Habel Okema, aliusifu mpango wa CHECKMATE na kusema imeweza kusiadia kutoa huduma za ukaguzi na ushikaji doria barabarani..

“Tunaamini kwamba mpango huu utaisaidia serikali kuhakikishia Wakenya usalama wao barabarani. Mashirika na kampuni ambazo zimetumia mpango huu zimepata ufanisi mkubwa na visa vichache vya utovu wa maadili miongoni mwa madereva wao,” akasema Bw Okema.

Mpango wa SWHAP hufadhiliwa na serikali ya Uswidi na umetumika katika  zaidi ya vituo 370 katika mataifa ya Botswana, DRC, Kenya, Mozambique, Namibia, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.