Michezo

Nuer ajinyakia binti wa ulimbwende

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO 

KIPA matata wa Bayern Munich, Manuel Neuer amezua gumzo kubwa nchini Ujerumani baada ya kujinasia penzi motomoto la kipusa tineja, Anika Bissel, mwenye umri wa miaka 19 pekee.

Neuer, 34, anaanza kulidokoa tunda la Anika miezi minne pekee baada ya kutemana rasmi na mkewe Nina ambaye kwa mujibu wa gazeti la The Sun, analandana sana na Anika.

Anika kwa sasa ni mwanafunzi wa masuala ya ulimbwende na fasheni jijini Munich na pia ni huchezea klabu ya handiboli ya Kuties, Ujerumani.

Nina, 27, alifunga pingu za maisha na Neuer mnamo 2017 na kwa sasa ameondoka katika kasri alimokuwa akiishi na mlinda-lango huyo jijini Munich na kurejea kwao Berlin, Ujerumani.

Ingawa Anika ana nyumba yake binafsi viungani mwa jiji la Munich, gazeti la udaku la Bunte nchini Ujerumani limesisitiza kwamba kipusa huyo amekuwa mgeni wa mara kwa mara katika kasri la Neuer ambaye ni miongoni mwa makipa wakwasi zaidi katika ulingo wa soka kwa sasa.

Akihojiwa na Bunte wiki iliyopita, Neuer alikiri kwamba tayari amemvisha Anika pete ya uchumba na kwa sasa anapanga kumtambulisha rasmi kwa mama yake, Marita, kabla ya kula naye yamini ya ndoa.

Christopher ambaye ni kakaye Anika, pia ni mchezaji mahiri wa handiboli katika kikosi cha HC Erlangen kinachoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani.

Neuer ambaye kwa sasa anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Chelsea, Uingereza, alianza kuvalia jezi za Bayern mnamo 2011 baada ya kuagana na Schalke, Ujerumani. Anajivunia kushindia Bayern mataji mengi ya haiba yakiwemo saba ya Bundeliga na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kipa huyo amewajibishwa na timu ya taifa ya Ujerumani mara 92 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyakua Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.