Dondoo

Nusra afutwe kazi kwa kuonja mlo wa mdosi

August 6th, 2018 1 min read

Na DENNIS SINYO

POLO mwenye tabia ya kuonjaonja chakula cha bosi wake, alijipata pabaya baada ya kupatikana peupe akiteremsha mchuzi wa nyama uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya mwajiri wake.

Jamaa huyo ambaye si mpishi, alikuwa na mazoea ya kuingia jikoni saa saba mchana kila siku.

Inasemekana alikuwa akitumia nafasi hiyo kuwachenga wapishi ili kupata nafasi ya kuonja mapochopocho wanayopikia mkubwa wa kampuni iliyokuwa imemwajiri.

Licha ya kupewa onyo mara kadhaa, jamaa hakukoma kabisa kuingia jikoni. Tabia hiyo iliwakera wapishi ambao waliamua kumripoti kwa msimamizi wao ili achukuliwe hatua kali kwani alikuwa amevuka mipaka.

Inasemekana kwamba jamaa huyo aliwekewa mtego bila kujua.

“Mdosi alikuwa amewaambia wapishi wamfahamishe punde tu baada ya jamaa kuingia jikoni. Jamaa alipokuwa akionja chakula ilivyokuwa kawaida yake, mdosi alidunda jikoni na kumfumania peupe,” alisema mdokezi.

Kalameni hakuamini macho yake alipomuona mdosi akimtazama kwa jicho la hasira.

“Kumbe ni ukweli unaonja chakula changu? Unajua kuwa kosa hilo linaweza kukufanya upoteze kazi yako?’’ alifoka mdosi.

Swali hilo lilimfanya jamaa kuishiwa na nguvu na kubakia mdomo wazi. Alilazimishwa kutafuna chakula chote wafanyikazi wengine wakimtazama kwa mshangao.

“Jamaa alishindwa kula chakula hicho na badala yake akapiga magoti kuomba msamaha kwa kosa hilo.

Mdosi wake alisema alikuwa amechoshwa na tabia ya jamaa akisema ilikuwa kinyume na kanuni za kampuni. “Tabia hii haikubaliwi katika kampuni yetu na sitaki kuona tena tukio hilo,” alichemka mdosi.

Jamaa aliinuka na kuondoka jikoni asiamini kwamba ulafi wake nusura umfanye amwage unga. Aliapa kutoingia jikoni tena huku wapishi wakipewa onyo la kutoruhusu yeyote kuingia humo kwa mara nyingine.