Habari Mseto

Nusu ya mapato hutumika kulipa madeni

October 4th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

SERIKALI inatumia zaidi ya nusu ya mapato yote nchini kulipia madeni, ripoti ya Hazina Kuu imefichua. 

Kati ya Sh100 zinazopatikana na Hazina Kuu Julai na Agosti, Sh57 zilitumiwa kulipa madeni.

Kutokana na kulipwa kwa madeni, serikali ilitumia Sh118.08 katika muda wa miezi miwili ya mwanzo katika mwaka huu wa kifedha kulipa madeni.

Katika kipindi kama hicho mwaka jana, serikali ilitumia Sh35.08 bilioni kulipa madeni. Waziri wa Fedha Henry Rotich alisema hayo katika ripoti ya hivi punde kuhusu mapato ya serikali.

Kiwango cha madeni kimekuwa cha juu kikilinganishwa na kiwango cha mapato ya serikali, hasa kutokana na kuwa mikopo iliyochukuliwa miaka mitano iliyopita imekomaa na imeanza kulipwa.

Kutokana na hilo, utoaji wa fedha kwa miradi umekuwa balaa ikizingatiwa kuwa kaunti 32 kati ya 47 hazikupokea mgawo wazo kutoka kwa serikali ya kitaifa katika kipindi hicho.