Nusu ya Wakenya hawajui chochote kuhusu BBI – Ripoti

Nusu ya Wakenya hawajui chochote kuhusu BBI – Ripoti

Na WANDERI KAMAU

KARIBU nusu ya Wakenya hawajui lolote kuhusu mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), licha ya serikali kutumia mabilioni ya fedha kuuendesha.

Inakisiwa kuwa kufikia sasa, serikali imetumia karibu Sh10 bilioni kuupigia debe mswada huo.

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na shirika la Trends and Insight for Africa (TIFA) jana, asilimia 47 ya Wakenya walisema hawafahamu lolote kuhusu mswada huo.

Utafiti unaonyesha kuwa licha ya juhudi hizo, ni asilimia sita pekee wanaoufahamu mswada huo kwa undani.

Kando na hayo, asilimia 31 ya Wakenya wanaupinga ikilinganishwa na asilimia 19 pekee wanaouunga mkono.

Kulingana na wadadisi, hilo huenda likawa pigo kwa serikali, ikizingatiwa kwamba imekuwa ikitumia karibu kila mbinu kuwarai wananchi kuiunga mkono.

Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 18 hawangeupigia kura mswada huo, huku asilimia 25 wakiwa hawajafanya maamuzi kuuhusu.

Wanaounga mkono wanataja kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti, kubuniwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Wadi (WDF), kubuniwa kwa maeneobunge mapya 70 kuwa miongoni mwa sababu zinazowaridhisha.

Hata hivyo, wale wanaoupinga wanataja kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti, matumizi ya fedha za serikali kuupigia debe, kubuniwa kwa nafasi za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili kati ya masuala mengine kama sababu za kuupinga.

Mchakato wa kubuni mswada huo ulianza Machi 2018, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuridhiana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kufuatia uchaguzi mkuu tata wa 2017.

Wafuasi wa Bw Odinga walizua fujo wakieleza kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo.

Muungano wa NASA, aliouongoza Bw Odinga ulisusia marudio ya uchaguzi huo ukidai Chama cha Jubilee (JP) kilikuwa na njama ya kuwaibia kura.

Ingawa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakisisitiza kuwa lengo la mchakato huo ni kuleta umoja nchini, juhudi zao zimekuwa zikipata pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi, hasa Naibu Rais William Ruto.

Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa TIFA, Bi Maggie Ireri, alisema matokeo hayo yanapaswa kuwafungua macho wanaoupigia debe mchakato huo kuhusu sababu ambazo huenda haziwaridhishi Wakenya.

Akaongeza: “Inaonekana matatizo yaliyojitokeza awali bado hayajawaridhisha wananchi licha ya mabadiliko kadhaa yaliyofanywa. Wengi wanaonekana kusukumwa na dhana kuwa mswada huo ni njama ya wanasiasa kujitengenezea nyadhifa za uongozi baada ya uchaguzi wa 2022.”

Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa kutumia fedha za umma kuuendesha mchakato huo, hasa shughuli ya kukusanya saini kabla ya kuwasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Rais Kenyatta pia alilaumiwa kwa “kuwahonga” madiwani ili kuupitisha mswada huo, baada ya kuwaahidi kugeuza mkopo wao wa magari kuwa ruzuku kutoka kwa serikali.

Naibu Rais William Ruto amekuwa akitaja mchakato kama njama ya viongozi kujifaidi na badala yake akisema kuwa kuna masuala muhimu yanayopaswa kushughulikiwa kwanza.

You can share this post!

‘Wanajeshi 11 walioangamia kwenye ajali ya helikopta...

Ruto aahidi wapiga kura bondeni uhuru wa kuamua