Habari za Kitaifa

Nusu ya waliofanya KCSE 2023 hawakuomba kujiunga na vyuo, ripoti yaonyesha

May 21st, 2024 1 min read

NA JAEL MAUNDA

ZAIDI ya wanafunzi 800,000 waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka jana, hawakutuma maombi ya kuendelea na elimu ya juu.

Taasisi inayohusika na kuwatunuku wanafunzi nafasi hizo, KUCCPS ilisema ni wanafunzi 895,232 pekee kati ya 1,780,806 waliotuma maombi hayo kati ya Februari 7 na Machi 4 mwaka huu.

Akizungumza katika jumba la Bima, South C, Nairobi jana, Afisa Mkuu Mtendaji Dkt Agnes Mercy Wahome alisema karibu asilimia 50 ya watahiniwa hawakuomba nafasi.

Baada ya matokeo ya KCPE kutangazwa, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alikuwa amewaomba machifu wawatafute watahiniwa 48,000 waliopata alama E, ili hata wao wajifunze ujuzi.

Kati ya waliotuma maombi, 258,935 watajiunga na vyuo vikuu nchini. Vyuo vya umma vilipata wanafunzi zaidi ikilinganishwa na vyuo vya kibnafsi.

“Idada ya wanafunzi wa kike imeendelea kuongezeka katika vyuo vya ufundi na sanaa ikilinganishwa na wanafunzi wanaume,” akasema Bi Wahome.