Habari Mseto

Nusu ya watahiniwa wa ualimu wafeli vyuoni

November 16th, 2018 2 min read

Na OUMA WANZALA

Takriban nusu ya walimu wote waliokuwa vyuoni na waliofanya mtihani mwaka huu wamefeli. Hali hiyo imeibua wasiwasi kuhusiana na ujuzi wa walimu wanaofuzu.

Hilo limetangazwa huku Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ikielezea hofu yake kuhusiana na kutohitimu kwa walimu katika masomo wanayofunza kote nchini.

Jumla ya walimu 10,457 kati ya 29,530 waliokuwa katika mafunzo watafanya mtihani tena mwaka ujao ikilinganishwa na 12,438 walioanguka mtihani mwaka jana.

Hali hiyo inamaanisha kuwa, walioanguka watakaa nje kwa muda kabla ya kufanya mtihani huo mwaka ujao.

Ni watahiniwa 21 pekee waliopata maki za juu zaidi katika mtihani wa walimu wa shule za msingi, miezi kadhaa baada ya Wizara ya Elimu kupunguza alama za kujiunga na taasisi za mafunzo ya walimu kutoka C hadi D kwa lengo la kuwafaa wananchi wa kaunti 17 ambazo hazina miundomsingi ya kutosha.

Taasisi za mafunzo za kibinafsi zilipata idadi kubwa zaidi ya walimu walioanguka mtihani huo.

Jumla ya watahiniwa 12,388 walipata alama za wastani ilhali wengine 5,581 walipita kwa alama za chini.

Jumla ya watahiniwa 807 (asilimia 2.69) ya watahiniwa wote hawakuwa wametimiza mahitaji ya kozi.

“Hii ni kwa sababu alama za mijarabu ya mara kwa mara za watahiniwa hao hazikuwasilishwa na taasisi ili kujumuisha alama zote,” ilisema ripoti ya Baraza la Kitaifa la Mtihani (KNEC).

Jumla ya watahiniwa 266 (asilimia 0.89) ya watahiniwa walioanguka watafanya tena mitihani yote mwaka ujao.

Mtihani wa PTE hufanywa na walimu wanaotaka kupata cheti baada ya mafunzo ya miaka miwili.

Ili kujiunga na taasisi ya mafunzo, lazima mwanafunzi awe na alama ya C kwa wale wasio na ulemavu na C – kwa walemavu (viziwi na vipofu).

Watahiniwa husoma masomo 14 na kufanya mitihani 21 na mazoezi ya kufunza kabla ya kufuzu.

Wakati wa mtihani wa PTE 2018, jumla ya watahiniwa 11,651 walikuwa wa kiume na 17,879 walikuwa wanawake ikilinganishwa na 10,402 (kiume) na 13,646(kike) mwaka jana.

“Hilo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 12.01 na 31.02 kwa wanaume kwa wake,” ilisema ripoti hiyo.

Idadi ya waliokalia mtihani huo iliongezeka kutoka 24,454 mwaka wa 2017 hadi 29,530 mnamo 2018, ambalo ni ongezeko la asilimia 20.76.

Katika muda wa miaka mitano, kumekuwa na watahiniwa wa kike wengi zaidi ikilinganishwa na wanaume.

Idadi ya waliopita mtihani kwa alama za chini na zaidi iliongezeka kwa asilimia 18.61 ikilinganishwa na 2017 ambapo idadi hiyo ilikuwa ni asilimia 10.30.