Dondoo

Nusura aachwe na gari akila uroda

December 2nd, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

SOTIK, BOMET

JOMBI aliyezuru mji huu kuhudhuria harusi nusura aachwe na basi kwa sababu alikuwa bado akishiriki fuska kwenye gesti.

Kulingana na mdokezi wetu, kulikuwa na hafla ya harusi eneo hili. Jamaa alikuwa miongoni mwa wageni waliofika kutoka mbali kwa basi ili kuhudhuria sherehe hiyo ya kukata na shoka.

Wakati sherehe ikiendelea, jombi alipatana na msichana ambaye alikuwa akimjua zamani. Baada ya kujuliana hali, wawili hao waliamua kufufua mahanjamu yao ya awali.

“Jamaa alimuomba demu amrambishe asali akisema hiyo ilikuwa nafasi yao ya kipekee. Lakini kipusa alichukua muda kujibu ombi hilo kabla ya kumkubalia jombi kukata kiu,” mdaku alisimulia.

Harusi ilipokuwa kileleni, wawili hao walionekana na watu wachache wakiondoka na kuelekea gesti moja kulishana uroda.

Sherehe ilikamilika na watu wakapanda basi kurudi makwao. Lakini mushkil ulitokea ilipojulikana kwamba abiria huyo barobaro hakuwa ameingia ndani ya basi.

“Jamaa alipigiwa simu na aliposhika alidai kwamba alikuwa karibu kufika kwa basi. Wengi waliteta na kulaani kitendo cha jombi huyo kutoweka, na kuwafanya wamsubiri kwa muda mrefu huku usiku ukibisha hodi,” mdokezi aliyekuwa katika sherehe hiyo alieleza.

Fununu zilichipuka kuwa jamaa alikuwa akila uroda, habari zilizowafanya watu kukasirika hata zaidi huku wengine wakiangua kicheko.

“Dereva aliamrishwa kungurumisha basi ili waanze safari ya kurudi nyumbani, naye hakusita kufanya hivyo.

“Lakini hatua chache tu polo alionekana akikimbia mbio huku anapiga kelele asiachwe. Kilichowafanya watu kuangua kicheko ni polo kuonekana akifunga zipu huku akijaribu kukimbia kufikia basi,” mdaku alisimulia.