Habari za Kitaifa

Nyakang’o amulika serikali kwa kutumia Sh70.41bn bila idhini ya Bunge

March 8th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto ilitumia Sh70.41 bilioni katika miradi ya maendeleo bila idhini ya Bunge katika miezi sita ya kwanza katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024.

Mdhibiti wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o mnamo Alhamisi aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango kwamba pesa hizo zilitumika kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM Act) 2012 inayosema kwamba sharti Bunge litoe idhini kabla ya serikali kutumia fedha.

Dkt Nyakang’o alielezea jinsi ambavyo wizara, idara na mashirika ya kiserikali yalitumia pesa hizo kugharimia shughuli za kila siku badala ya maendeleo.

“Inasikitisha kuwa jumla ya Sh70.41 bilioni zilitumika na serikali kuu katika kipindi cha miezi sita bila idhini ya Bunge, hali ambayo inakiuka kipengele cha 223 cha Katiba,” Dkt Nyakang’o akaambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani.