Habari Mseto

Nyakundi akamatwe, mahakama yaagiza

April 22nd, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Mahakama ya Milimani imetoa kibali cha kumkamata mwanablogu Cyprian Nyakundi kwa kuchapisha habari za uwongo kuhusu mazishi ya kisiri aliyekuwa afisa mkuu wa Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) Bw Antony Gichira.

Nyakundi alidai Bw Gichira aliaga kutokana na maradhi ya corona na kuzikwa kisiri. Hakimu mkazi Catherine Muthoni Nzibe (pichani) aliruhusu Bw Nyakundi atiwe nguvuni na kufikishwa kortini Mei 14.

Kiongozi wa mashtaka Patience alinweleza hakimu kuwa Bw Nyakundi alitakiwa afike kortini Jumanne kujibu shtaka la kuchapisha habari za uwongo kuhusu kifo cha Gichira.

Mahakama ilielezwa kuwa Nyakundi alitiwa nguvuni wiki tatu zilizopita kisha akaagizwa na hakimu mwandamizi Bernard Ochoi afike kortini Aprili 21.

Kiongozi wa mashtaka Patience Mbange. Picha/ Richard Munguti

“Naomba hii mahakama itoe kibali cha kumtia nguvuni Nyakundi kamwa kutofika mahakamani kujibu shtaka kama alivyoagizwa,” Mbange alimsihi hakimu.

Alisema Nyakundi alizuiliwa kwa siku tatu kisha akaachiliwa kwa dhamana. Mahakama ilifahamishwa alitarajiwa afike kortini.

Mahakama ilifahamishwa mshukiwa anatakiwa kushurutishwa asiendelee kuchapisha habari za kufedhehesha mamlaka ya ushuru.

Akitoa uamuzi hakimu aliamuru Nyakundi akamatwe na afisa wa polisi Isaac Tenai.