Habari Mseto

Nyama ya mbuzi haina ladha tena, anawala vinyonga, kobe, mbwa na paka

May 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU
 
MWANAMUME anayefanya kazi ya ubawabu kutoka kijiji cha Ogongo, eneo la Nyatike, Kaunti ya Migori, ameshtua Wakenya baada ya kuanzisha ufugaji wa vinyonga, mijusi na wazee kobe, si wa kuuza ama kazi nyingine, ila wa kula.
 
Thomas Odembo mwenye umri wa miaka 35 anasema kuwa alianza kula vinyonga, mijusi, kobe, paka na mbwa baada ya kufanya kazi na mkandarasi kutoka China.
 
Baba huyo wa watoto saba anasema kuwa ana hamu kubwa ya kula nyama hizo ambazo si za kawaida, jambo ambalo lilimsukuma kuanza kufuga wanyama hao nyumbani kwake, kama mbinu moja ya kujiundia lishe yake.
 
“Nimepoteza hamu ya kula nyama za ng’ombe na mbuzi na niko tayari kusambazia wanakijiji nyama hii tamu,” akasema Bw Odembo.
 
Jumatano, mwanamume huyo alikuwa akiandaa kobe kwa chakula cha mchana baada ya kumchinja, akisema kuwa “jana usiku (Jumanne) nilikula kinyonga, huyu kobe aliletwa na jirani ambaye alimpata katika shamba.”
 
Aliendelea kuhadithia: “Nimefanya kazi na wakandarasi kadhaa wa kutoka China ambapo nilijifunza kuhusu lishe hii nilipoona kuwa wanawala wanyama hawa watamu na hawawadhuru.”
 
Alisema kuwa nyama za wanyama hao zinaonja kama zile za kawaida tu.
 
Bw Odembo ni mzaliwa wa Kasigunga, Kaunti ya Homa Bay na anafanya kazi na kampuni kutoka China katika eneo la Nyatike, Migori.
 
“Nyama niipendayo sana ni ile ya nyoka, kisha mijusi, vinyonga na kobe,” akasema.
 
Hata hivyo, ni yeye tu anayekula wanyama hao katika familia yake, kwani mkewe na wanao hawali kabisa.