Habari Mseto

Nyamira yashinda Kisii kesi kuhusu mji wa Keroka

February 15th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MAHAKAMA ya Ardhi na Mazingira imezitaka kaunti za Nyamira na Kisii kukoma kuzozania mji wa Keroka.

Jaji Mugo Kamau wa mahakama hiyo amesema Alhamisi kuwa inajulikana wazi ni wapi kuliko mipaka ya Nyamira na ile ya Kisii katika mji huo wa mpakani na hivyo basi, serikali za kaunti hizo zinafaa kuiheshimu katika ukusanyaji kodi na utoaji huduma.

Mnamo Aprili 2023, diwani wa Rigoma Nyambega Gisesa aliwasilisha kesi mahakamani akiituhumu serikali ya Kisii kwa kukusanya ushuru katika maeneo ambayo ni ya Nyamira.

Katika kesi yake, diwani huyo ambaye ni mwanahabari, aliitaka mahakama kuweka wazi kuliko mipaka baina ya kaunti hizo.

Ili kumsaidia kibarua hicho, Jaji Kamau alitafuta maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), maafisa wa Tume ya Ardhi Nchini (NLC) na masoroveya wengine kubaini kuliko mipaka hiyo.

Maafisa hao waliuzuru mji wa Keroka na kuweka vigingi kote kote kuonyesha mipaka hiyo.

Vigingi hivyo viliingia katika maeneo ambayo kwa miaka mingi yalihesabiwa kama Kisii.

Ripoti iliyoaandikwa na masoroveya hao ndio aliyoitumia jaji Kamau kutoa uamuzi wake.

“Kufuatia ripoti hiyo, mipaka inajulikana na inafaa kuzingatiwa,” jaji Kamau akasema huku akiwataka watu wa jamii ya Abagusii kuishi kwa amani.

“Jamii hii ni ya watu ambao wameishi kwa amani kwa miaka mingi. Mambo ya mipaka hayafai kuwatenganisha watu wa Nyamira na Kisii kwa sababu ni wa jamii moja,” jaji aliongeza huku akifananisha mzozo huo na mwanamwali anayemezewa mate na wanaume wawili.

Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo aliyekuwa mahakamani, alitaja uamuzi huo kama ushindi kwa watu wa Nyamira.

“Huu ni ushindi kwetu. Jinsi ilivyosema mahakama, huu si wakati wa mvutano bali ni wa kufanyia watu wetu maendeleo,” gavana Nyaribo akasema.

Huku mawakili wa serikali ya Nyamira wakifurahia uamuzi huo, wale wa Kisii wakiongozwa na Hillary Tom Ongori walisema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

“Hatujafurahia uamuzi huu. Bado mapambano na tutakata rufaa,” wakili Waikiki Ongori akasema.