Kimataifa

Nyani anyang'anya mwanamke mtoto na kumuua!

November 16th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

WAKAZI wa kijiji kimoja nchini India wamebaki katika hali ya huzuni na mshangao, baada ya nyani kuingia katika nyumba moja, kumnyang’anya mama mtoto na kumuua kisha kumwacha katika paa ya nyumba ya jirani.

Nyani huyo anadaiwa kumnyanganya mama mtoto wake wa siku 12 alipokuwa akimnyonyesha ndani ya nyumba, kisha kumuuma na kumjeruhi vibaya alipotoroka naye nje.

Tukio hili la kushangaza lilishuhudiwa katika Jiji la Agra, Kaskazini mwa India.

Ilidaiwa kuwa nyani huyo alimwachilia mtoto mwenyewe tu baada ya majirani kufika na kumfukuza, ndipo akamwacha juu yap aa ya nyumba ya jirani.

Mtoto huyo mvulana hata hivyo aliaga dunia baadaye alipokuwa akitibiwa kutokana na majeraha aliyopata kwa kuumwaumwa na nyani huyo katika hospitali ya eneo hilo.

“Nyani huyo alimuuma mtoto kichwani na kumwachilia tu wakati wakazi walimfukuza kwa vijiti na kumtupia mawe,” akasema Ajay Kaushal, afisa wa polisi msimamizi katika kituo jirani.

Hiki kilikuwa kisa cha hivi punde zaidi kati ya vingi kuhusu mavamizi ya nyani eneo hilo.

Miezi miwili iliyopita mtoto mwingine alivamiwa na wanyama hao na kujeruhiwa vibaya, hadi sasa bado anatibiwa. Vilevile, mwanaume aliyekuwa kwenye pikipiki aliuawa na wanyama hao.

“Nyani wako kila mahali Agra,” akasema Shravan Kumar, mwanaharakati wa kimazingira eneo hilo “Wao huja kutafuta chakula lakini wanaiba na kuvamia watu vilevile.”