Habari

Nyani wahangaisha wakazi majumbani

January 28th, 2020 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

WAKAZI wa maeneo ya Lake View, Flamingo, Kaloleni na Racecourse katika Kaunti ya Nakuru wanaishi kwa hofu kutokana na kero la nyani wanaoingia kwenye nyumba zao.

Maeneo hayo yanayopakana na mbuga ya wanyama ya Nakuru, yamezidi kushuhudia matatizo ya kila mara na wanyama pori.

Kulingana na wakazi hao, bidhaa nyingi za nyumbani kama vile za elektroniki, vyakula na mimea shambani vimeharibiwa na nyani hao ambao wamezidi kusumbua kwa muda mrefu.

Bw Clement Njuguna, mzee wa mtaa wa Lake View anasema chanzo kikuu cha nyani hao kutoroka mbugani ni kwa sababu ya uharibifu wa misitu ambao unashuhudiwa.

Wengi wa nyani hao wanasemekana kuwa na maarifa kuhusu jinsi ya kuvuka nyaya za stima ambazo zimetumika kwenye ua wa mbuga lao.

“Wajua ni nyaya zipi zinazopitisha nguvu za umeme na zipi ambazo haziwezi kudhuru. Wanajua pia wakati wa kuingia kwenye maboma ya watu na wakati gani wa kuondoka,” akasema Njuguna.

Wakazi wanasema ukosefu wa vyakula mbugani ni baadhi ya chanzo cha wanyama hao wasumbufu kutoroka mle ndani na kuvuruga watu kwenye makazi yao.

Bw Ahmed Yusuf, mkazi wa Racecourse alisema alifuga mbwa nyumbani kwake ili amsaidie kuogopesha nyani hao kufika kwake lakini hilo halijasaidia.

“Nilishangaa kuona jinsi nyani wawili wa kiume walivyovuka uzio wa makazi yangu na kumvamia mbwa wangu kabla ya kupiga kambi wakijaribu kupenyeza ndani ya nyumba,” akasema Bw Yusuf.

Aliongeza kuwa kila wanapofika, nyani hao huingia ndani ya nyumba za wakazi kwa fujo na kutafuta aina yoyote ya vyakula.

“Wakikosa, wao huharibu vyombo na kusababisha hasara kubwa,” akasema.

Bi Rhoda Murimi, mkazi wa Kaloleni alisema hivi maajuzi alikumbana na kundi la nyani ambao walifika kwake wakati wa maakuli ya jioni.

“Nilikuwa nje nikipika kutumia jiko la makaa. Kwa ghafla wakaja nyani sita ambao walitumia nguvu kunivuruga kabla ya kumwaga maji yaliokuwepo jikoni na kutoroka na ndoo ya unga wa ugali.” akasema.

Mkazi mwingine John Kioko alisema watoto na kina mama ndio huumia sana wakati wa mvutano kati ya nyani na binaadamu. Alisema nyani huogopa kuingia kila wanapowaona wanaume na kwamba huonyesha hasira na kutaka kuanzisha vita wanapofukuzwa.

Chifu wa eneo hilo Bw George Ng’ang’a alisema kuwa idara ya kushughulikia wanyama pori (KWS) imefahamishwa kuhusu habari hizo lakini swala hilo halijawai kupata suluhu ya kudumu.

“Mara kwa mara mimi binafsi nimehakikisha kuwa KWS wanapata habari hizi lakini shida hii haijawahi kupata suluhu. Kila mara wao hutwambia kuwa tutahadhari na kuonya wakazi dhidi ya kuwauwa wanyama pori,” akasema Bw Chifu.

Aliomba serikali ya kaunti kuingilia kati na kuhakikisha kuwa raiya wanaepushwa na jinamizi hilo.