Habari Mseto

Nyanya, 76 afariki baada ya kukosa kumtumbuiza Rais Kisumu

December 18th, 2018 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

MWANAMKE aliyekosa nafasi ya kumtumbuiza Rais Uhuru Kenyatta kwenye ziara yake jijini Kisumu majuzi alizimia na kufariki Jumatatu.

Familia ya mwanamke huyo, aliyetambuliwa kama Wilfrida Abwajo mwenye umri wa miaka 76, ilisema alifariki kutokana na mshtuko aliopata baada ya kunyimwa nafasi hiyo.

Kulingana na Bi Pamela Ogal, ambaye ndiye mwenyekiti wa Kundi la Wanawake la Oruba, linalojumuisha Wachezaji Densi wa Kitamaduni wa Dodo, walikuwa wamealikwa na Waziri wa Utalii na Utamaduni wa Kaunti ya Kisumu Achie Alai.

Alisema kuwa waliteuliwa kuwa miongoni mwa watu ambao wangemtumbuiza Rais Kenyattta kwenye ziara hiyo, baada ya kushiriki katika hafla za sherehe ya Sikukuu ya Jamhuri mnamo Jumatano iliyopita.

“Tuliunganishwa na waziri huyo na aliyekuwa diwani wa Wadi ya Kolwa Mashariki Robert Otuge. Baadaye waziri huyo alituahidi kwamba angetuunganisha na Kikosi cha Kumtumbuiza Rais (PPMC) ili kupata nafasi ya kumtumbuiza pamoja na wageni wengine. Tulifanikiwa kufika alikokuwa Rais mwendo wa saa mbili asubuhi bila kuchelewa, ila hatukupata nafasi ya kumtumbuiza,” akasema Bi Ogal.

Hata hivyo, Bi Alai alijitetea vikali akisema kuwa kitengo cha Rais ndicho kinachopanga na kuamua wale ambao hutumbuiza katika hafla zake. “Hili ni jukumu la PPMC. Tulichagua makundi 30 ya muziki na kuyakabidhi kitengo hicho. Hata hivyo, ndicho chenye uamuzi wa mwisho kuhusu wale wanaopaswa kutumbuiza,” akasema Bi Alai.

Kwa upande wake, PPMC ilisema kuwa watumbuizaji wote ambao walimtumbuiza Rais siku hiyo walilipwa. Kwenye taarifa, mwakilishi wa kitengo hicho Donald Otoyo alisema kwamba watumbuizaji wote wanaoalikwa na serikali za kaunti huwa wanashughulikiwa na serikali husika ya ugatuzi wala si serikali kuu.

“Kulingana na taratibu zilizopo, watumbuizaji wote wanaoalikwa na serikali za kaunti wanapaswa kulipwa nayo kulingana na makubaliano kati yao. Hakikisho hili lilitolewa na afisi ya gavana na afisa wa utamaduni wa kaunti aliyekuwepo. Nitatoa maelezo zaidi,” akasema Dkt Otoyo, kwenye mazungumzo na ‘Taifa Leo.’

Marafiki wa marehemu walisema kuwa alijitolea kuwaongoza wanawake 15 wa kundi la Oruba kufanya mazoezi kwa matumaini kwamba wangepewa nafasi ya kutimiza ndoto yao ya kutumbuiza Rais. Vikundi mbalimbali vilimtumbuiza Rais wakati akizindua Majaribio ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) uwanjani Mamboleo.