Habari Mseto

Nyanya auawa kwa kushukiwa kutumia uchawi kuua watu 4

March 27th, 2018 1 min read

Na NICHOLAS KOMU

NYANYA mwenye umri wa miaka 60 aliuawa na wakazi wa kijiji cha Kibingoti, Kaunti ya Kirinyaga kwa kushukiwa kutumia uchawi kusababisha ajali ya barabarani ambapo watu wanne wa familia moja walikufa mnamo Jumamosi.

Mwanamke huyo kwa jina Wakiini Musa aliuawa na wakazi waliodai kwamba alitumia uchawi kusababisha ajali iliyotokea eneo la Marua kwenye barabara ya Nyeri kwenda Karatina. Ajali hiyo ilihusisha gari la serikali na lori lililobeba soda.

Kulingana na baadhi ya wakazi, mwanamke huyo, ambaye amekuwa akizozania ardhi na familia ya waliokufa, alisikika akisema wangeangamia mmoja mmoja kwa kujaribu kumuondoa kutoka ardhi wanayozozania.

Saa chache baada ya kutoa matamshi hayo, watu sita wa familia hiyo walihusika kwenye ajali na watatu wakafa papo hapo. Mtu wa nne alikufa Jumatatu akiendelea kupata matibabu.

“Alisikika akiwaambia kuwa wangeanza kufa mmoja baada ya mwingine. Siku hiyo, watu watatu wa familia hiyo walikufa kwenye ajali ya barabarani,” alisema mkazi Bw Joseph Maina.

Miongoni mwa waliokufa kwenye ajali hiyo ni ndugu wawili ambao walikuwa wakimpeleka mama yao katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Nyeri. Mama yao pia alikufa kwenye ajali hiyo.

Ingawa wengi wanaweza kusema matamshi ya mwanamke huyo na kutokea kwa ajali hiyo saa chache baadaye ni sadfa tu, wakazi wanaamini kwamba aliwaroga ili wahusike kwenye ajali.

Walimvamia kwa rungu, fimbo na panga mwendo wa saa nane Jumapili usiku na kumpiga hadi wakamuua.

Mkuu wa polisi wa Kirinyaga Magharibi (OCPD) Sicily Gatiti alisema wanawasaka waliotekeleza mauaji hayo akieleza hawatakubali watu kuchukua sheria mikononi mwao.