Habari Mseto

Nyanya wa miaka 73 apatikana amenyongwa nyumbani kwake

June 19th, 2018 1 min read

Na Ndung’u Gachane

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 73 kutoka kijiji cha Kigoro, lokesheni ya Maragua Ridge, Kaunti ya Murang’a alipatikana ameuawa Jumapili usiku. Wakazi walipata mwili wa Jedida Wambui Muthengi karibu na nyumba yake. Wakazi hao walisema aliuawa kwa kunyongwa.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, John Onditi, alisema polisi wanachunguza kifo cha nyanya huyo. Bw Onditi aliwaomba wakazi kushirikiana na polisi kwa kutoa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa washukiwa

Bw Ng’ethe Magua, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, alisema nyanya huyo alikuwa akiuza matunda katika steji ya Mbombo na alikuwa akifika nyumbani mwendo wa saa tatu usiku.

Bw Magua alisema mwanamke huyo alikuwa akiishi peke yake kwa sababu watoto wake watano wameoa na wengine wameenda kutafuta kazi nje ya Kigoro.

“Marehemu Wambui alinyongwa na hii inaweza kuthibitishwa na kamba iliyopatikana shingoni mwake. Aliyemuua alimfunika mdomo kwa kitambaa,” alisema Bw Magua.