Habari Mseto

Nyanya yangu hakunifunza kuwa kula uroda ni hatia, mshukiwa amwambia hakimu

February 28th, 2018 1 min read

Godfrey Mungai Waweru akiwa kizimbani katika mahakama ya Milimani, Nairobi alipohukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa ubakaji. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME mwenye umri wa miaka 50 alimshangaza hakimu mkuu Francis Andayi katika mahakama ya Milimani, Nairobi alipomweleza kwamba nyanya yake aliyemlea hakumshauri kwamba kuoja ‘tunda la Edeni’ bila idhini ni hatia.

Akijitetea, Godfrey Mungai Waweru alisema, “Namlaumu nyanya yangu aliyenilea kwa kutonipa wosia kwamba kula tunda la Edeni bila idhini ni hatia kisheria. Naomba hii mahakama msamaha. Nakusihi hakimu uamuru nitumikie kifungo cha nje kwa vile nimekaa gerezani kwa miaka mingi. Nimejutia tendo langu la kijinga na upumbavu.”

Waweru alipatikana na hatia ya kumbaka weita anayefanya kazi katika hoteli moja Nairobi aliyemvizia akitoka ndani ya matatu baada ya kazi katika eneo la Ngong.

Mshtakiwa alimshika mlalamishi mkononi na kumpeleka msituni kwa lazima na kumdhulumu kimapenzi.

Mlalamishi alimpigia simu pasta wa kanisa lao ambaye alimpeleka Hospitali ya Nairobi Women.

Hakimu alisema mlalamishi alikaguliwa kiafya na kupatikana amechafuliwa kingono.

“Tendo ulilomfanyia mlalamishi ni la kumshusha hadhi na lilikuwa la kidharau,” alisema hakimu.

Hakimu Andayi aliendelea kumweleza kwamba sheria inawalinda wasichana na kina mama dhidi ya watu kama  yeye (Waweru) walio na tabia za kihayawani.

Kwa sasa, Bw Waweru ataozea jela kwa miaka kumi kuhusu kitendo hicho.