Habari Mseto

Nyanza kuvuna zaidi kutokana na muafaka

February 23rd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MUAFAKA wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga umezidi kulizalia eneo la Nyanza matunda, kwani sasa Jiji la Kisumu litakuwa mwenyeji wa kongamano la awamu ya tisa la UN na serikali za Afrika ‘Africities’, mnamo 2021.

Kongamano hilo huwa kubwa na huvutia maelfu ya watu na hivyo kuandaliwa kwake Jijini Kisumu kutakuwa na manufaa makubwa, haswa ya kibiashara.

Ijumaa, Bw Odinga pamoja na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Kisumu walisema kuwa tayari maandalizi ya kongamano hilo yameanza, kwa ujenzi wa barabara na miundomsingi na usafishaji wa Ziwa Victoria kwa kuondoa magugumaji.

“Kuondolewa kwa magugumaji na miradi mingine inayoendelezwa ni baadhi ya maandalizi ambayo yanafanywa kwa ajili ya kongamano la Africities,” akasema Bw Wamalwa.

Tayari, Bw Odinga, Bw Nyong’o, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju, Waziri wa Utalii Najib Balala na wa Mazingira Keriako Tobiko wamefika Kisumu siku kadha zilizopita ambapo walianzisha mchakato wa maandalizi ya kongamano hilo.

Bw Odinga alisema Ijumaa Bw Wamalwa na Prof Nyong’o walimtembelea katika ofisi yake iliyopo Capitol Hill, Nairobi kumfahamisha namna maandalizi ya kongamano hilo yanaendelea.

Hadi kufikia 2021, maandalizi yatakayofanywa yatakuwa yamegeuza sura ya Jiji la Kisumu, kwa kurahisisha usafiri wa majini na barabarani na kuinua biashara katika eneo la ziwa Victoria.

Hii si mara ya kwanza kwa eneo pana la Nyanza kuvuna matunda ya muafaka tangu Machi mwaka uliopita, kwani Jumatano Rais Kenyatta na Bw Odinga pamoja na viongozi wengine wa serikali walikuwa kaunti ya Kisii, ambapo walizindua kuanza kuinuliwa kwa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kaunti ya Kisii.

Aidha, Desemba 2018 Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga walifanya ziara ya kihistoria eneo la Nyanza kwa siku mbili, ambapo walizindua mradi wa afya kwa Wakenya wote (UHC).