Makala

NYARIKI: Kuomba radhi kwa kutohudhuria mkutano ni udhuru, si rambirambi

February 25th, 2020 2 min read

NA ENOCK NYARIKI

NENO rambirambi linapotumiwa katika sherehe za matanga au mazishi, taswira ya kwanza inayojisawiri katika mawazo ya wanaozungumziwa ni mchango au pesa zinazotolewa kwa ajili ya kuwafariji makiwa kwa msiba wa mauti.

Aghalabu mchango huo hutolewa kwa niaba ya mtu ambaye hafiki kwenye sherehe ili kuwafariji wafiwa kwa sababu mbalimbali. Mchango au pesa hizo hufanya kazi ya udhuru kwa mfadhili.

Kwamba ijapokuwa hakufika kwenye mazishi au matanga angali anaomboleza na waliofikwa na msiba.

Maana ya pili ya neno hilo ilivyozoeleka katika sherehe hizo ni ujumbe wa faraja unaoandikwa na mtu fulani ili usomwe kwa wafiwa kwa niaba yake.

Hatimaye, hutumiwa na waombolezaji kwa maana ya mchango wanaoutoa ili kuwafaa wafiwa kugharimia mazishi.

Baadhi ya watu hulitumia neno rambirambi kwa maana ya ujumbe au salamu zinazotolewa na wale ambao hawakufika katika sherehe fulani ili zisomwe kwa hadhira kwa niaba yao.

Mathalani, katika kikao cha kupigia upatu maridhiano ya kitaifa kilichofanyika Narok, gavana mmoja alisema kuwa wenzake ambao hawakuhudhuria mkutano huo walikuwa wametuma rambirambi zao!

Matumizi ya neno hilo nje ya muktadha wa mazishi au matanga yamkini yanatokana na sababu mbili. Awali neno hilo lilitumiwa pia kwa maana chanya.

Kwenye toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno rambirambi limepewa maana mbili. Kwanza, ni tamko la kuonyesha masikitiko kwa maafa yaliyomfika mtu. Pili, ni tamko linaloonyesha furaha kwa mafanikio yaliyopatikana.

Hata hivyo, maana hii ya pili haijitokezi kwenye kamusi za punde zaidi. Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kuwa rambirambi ni maneno ya kuwaliwaza wafiwa yanayotolewa wakati wa msiba kwa kufiwa na jamaa yao. Maana inayokaribiana na hiyo inajitokeza katika Kamusi Elezi ya Kiswahili.

Sababu ya pili inatokana na kuhamishwa kwa neno ‘ujumbe’ kwenye kijelezi ujumbe wa faraja unaotolewa kwa wafiwa kwenye sherehe ya mazishi au matanga.

Kwa hivyo, neno hilo hutumiwa kwa maana ya ujumbe unaopelekwa katika sherehe zozote zile na wale ambao hawakuhudhuria sherehe hizo. Ndivyo alivyolitumia gavana tuliyemtaja.

Alhasili, shughuli au jambo muhimu linalotokea ghafla na kumfanya mtu asitimize jambo jingine alilokusudiwa kufanya ni udhuru.

Kwa hivyo, aliyekosa kuhudhuria mkutano fulani kwa sababu ya kutingwa na shughuli nyingine muhimu hupeleka udhuru bali si rambirambi. Matumizi ya neno la pili yanaegemea sherehe za mazishi na matanga.