Makala

AKILIMALI: Nyasi aina ya Brachiaria ni muhimu kwa ng’ombe wa maziwa

August 14th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NG’OMBE mwenye afya bora humfanya mfugaji kutabasamu na kufurahia kupitia uzalishaji wa maziwa na nyama.

Hayo yanajiri ikiwa mkulima anajali maslahi ya mifugo wake, kwa kuzingatia vigezo kadha wa kadha.

Ukimtunza ng’ombe vyema, hatakuwa na budi ila kukupa mazao ya kutosha na ya kuridhisha.

Mosi, hakikisha mazingira wanamoishi ng’ombe wako ni salama dhidi ya magonjwa na vimelea.

Chanjo, kuwapa dawa ya minyoo, kuwapulizia dawa ya kuua kupe na viroboto, ni programu muhimu kuzingatia katika ufugaji.

Kimsingi, ni muhimu mkulima ahakikishe ana daktari au mtaalamu wa mifugo kumuelekeza ili kuimarisha shughuli za ufugaji, hasa ng’ombe wa maziwa.

Mbali na kuhakikisha mifugo ni salama, kuna hili suala la lishe ambalo kwa kiasi kikuu huchangia kiwango cha uzalishaji kuwa bora au duni.

Wakulima waliofanikisha shughuli za ufugaji hususan wa maziwa, hutilia mkazo chakula wanachowapa ng’ombe.

Kumekuwa na malalamishi ya chakula duni cha madukani, kinachodaiwa kutoafikia ubora wa bidhaa, katika kisa hiki lishe isiyo na madini faafu na kamilifu ya mifugo na kuku.

Kulingana na wataalamu wa mifugo, ng’ombe wanapaswa kulishwa chakula chenye madini kamilifu.

Katika maghala ya wafugaji gwiji, hutakosa kutazama chakula aina ya hay na silage, wengi wakikumbatia mkondo wa kujiundia chakula.

Chumvi ya mifugo na molasses, pia huiweka kwenye orodha mahitaji muhimu kwa ng’ombe.

Aghalabu, wanaofahamu ubora wa chakula, wanajikuzia nyasi kama vile mabingobingo (Napier), Boma Rhodes na pia mahindi.

“Kujiri kwa nyasi aina ya Brachiaria, kumesaidia kuimarisha shughuli za ufugaji. Ng’ombe wanaweza kulishwa zikiwa kijani au kutengeneza silage na hay,” Wachira Ngure, mtaalamu anaeleza.

Isitoshe, ni aina ya nyasi zenye madini tele na zinazosifiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji hasa kwa ng’ombe wa maziwa.

“Brachiaria ina zaidi ya asilimia 18 ya protini. Ni bora katika mifugo wa maziwa na nyama,” anasema Anne Wangechi, mkulima wa nyasi hizo Mukurwe-ini, Kaunti ya Nyeri.

Kando na kukuza nyasi hizo kulisha ng’ombe wake, Anne amezigeuza kuwa kitega uchumi ambapo huzalisha katika kipande cha shamba chenye ukubwa wa ekari moja. Mkulima huyo anasema ekari moja huzalisha kati ya tani 18 – 20.

Chakula kingine bora kwenye ng’ombe wa maziwa ni desmodium, calliandra na lucerne.

Unahimizwa kuwa na mashine ya kusaga chakula cha mifugo.

Aidha, unapowatilia lishe kiwango cha usafi wa vifaa kinapaswa kuwa cha hadhi ya juu.

Madini, chumvi na maji ni viungo muhimu katika ng’ombe wa maziwa.

Ili kuzalisha maziwa ya kutosha, ya kuridhisha na bora, nywesha ng’ombe maji mengi na safi.