Michezo

Nyayo Stadium kufunguliwa na Rais Kenyatta hapo Septemba 26

September 25th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

UWANJA wa kitaifa wa Nyayo hatimaye unatarajiwa kufunguliwa na Rais Uhuru Kenyatta hapo Septemba 26, miaka mitatu baada ya kufungwa kufanyiwa ukarabati.

Barua kutoka kwa Kamishna wa Michezo, Gerald Gitonga imethibitisha Ijumaa kuwa Rais Kenyatta atafungua uwanja huo unaobeba mashabiki 30, 000.

“Rais wa Jamhuri ya Kenya ataongoza hafla ya kufungua uwanja wa Nyayo hapo Septemba 26 kwa hivyo tunaalika shirikisho lako kuhudhuria hafla hiyo muhimu ya wanamichezo. Tafadhali mwaliko huu uwafikie wachezaji pia,” alisema Gitonga katika barua yake na kutaka walioalikwa kufika katika uwanjani humo wakiwa wamevalia mavazi ya timu ya taifa.

“Washiriki wote watahitajika kuwa uwanjani kufikia saa tatu na nusu asubuhi Ijumaa,” barua hiyo ilisema.

Uwanja wa Nyayo ulifungwa mwaka 2017 ufanyiwe ukarabati kabla ya mashindano ya soka ya wachezaji wanaocheza barani Afrika katika mataifa yao almaarufu CHAN. Kenya ilifaa kuandaa mashindano ya CHAN mwaka 2018, lakini yakahamishiwa nchini Morocco baada ya viwanja kukosekana. Uwanja wa Nyayo pia haukuwa tayari.

Uliwahi kufunguliwa mwezi Agosti 2017 kwa mechi kubwa kwenye kalenda ya soka ya Kenya kati ya mahasimu wa tangu jadi Gor Mahia na AFC Leopards almaarufu ‘mashemeji derby’ na kufungwa tena kuendelea kufanyiwa ukarabati.

Uwanja huu, ambao ulitumiwa kwa mechi nyingi za Ligi Kuu ya Soka Kenya kabla ya 2017, ulifunguliwa tena kidogo kwa mbio za Beyond Zero mnamo Machi 8 mwaka 2020.

Mbio hizo ni mradi wa Mama Taifa Margaret Kenyatta zinazolenga kuimarisha afya ya kina mama na watoto pamoja na kupunguza maambukizi ya ukimwi kwa watoto. Vilevile, Nyayo ilifungwa Februari 11 kwa shughuli za kuomboleza rais wa pili wa Kenya, Daniel arap Moi.

Shughuli ya kwanza ya kimichezo kuandaliwa uwanjani Nyayo itakuwa mbio za kupima utayari wa Kenya kuandaa duru ya mwisho ya mbio za dunia za Continental Tour hapo Septemba 26. Duru hiyo maarufu kama Kip Keino Classic itaandaliwa Oktoba 3 ikivutia wakimbiaji zaidi ya 120 kutoka zaidi ya mataifa 30.