Habari Mseto

Nyeri kupata kiwanda cha maparachichi

June 4th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

GAVANA Mutahi Kahiga amesema serikali ya kaunti ya Nyeri inapania kuunda kiwanda cha maparachichi ili kupiga jeki ukuzaji wa zao hili.

Amesema hatua hii pia inalenga kufanya maparachichi kuwa miongoni mwa mazao yanayoingizia wakulima mapato.

Akizungumza Jumatatu akiwa Nyeri, Gavana Kahiga amesema mradi huu umepangiwa kugharimu kiasi cha Sh50 milioni.

“Wakulima eneo hili wamekuwa wakitegemea majanichai na kahawa, mazao ambayo hayajakuwa yakiwalipa vizuri. Tumeanza kuwekeza pakubwa katika kilimo cha maparachichi kwa sababu yana soko zuri ndani na nje ya nchi. Hayachukui nafasi kubwa ya shamba,” amesema Kahiga.

Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, Serikali ya Kaunti ya Nyeri imeonekana kuwa katika mstari wa mbele kuhimiza wakulima humo kuvalia njuga ukuzaji wa matunda haya.

Aidha, imekuwa ikisambaza miche kwa wakulima bila malipo sawa na kaunti ya Murang’a.

“Kiwanda hicho kitakuwa cha kusindika; kuyasafisha, kuchagua na kuyapakia ili kuuzwa nje ya nchi,” amefafanua, akidokeza kwamba kitajengwa eneo la Kiawaiganjo.

Aprili 2019 Kenya ilitia saini mkataba wa kuuza maparachichi nchini China.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mpango huo utasaidia kuinua kilimo cha avocado hapa nchini.

Ni hatua ambayo ilikabirishwa vyema na Wakenya, hasa wakulima.

Hata hivyo, kuna baadhi ya waliozua mjadala wakihoji mikakati maalum iwekwe ili kufanikisha mpango huo ili kuepuka kupunjwa na mawakala.

“Serikali inapaswa kuwa na miungano itakayoleta pamoja wakulima wa maparachichi ili wasipunjwe na mawakala. Itakuwa rahisi mazao yao kukusanywa na kuuzwa China,” anapendekeza Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda.

Mdau huyu pia anahimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika (Sacco) ili kuwatafutia soko la mazao yao. Bw Mwenda anapongeza serikali ya kaunti ya Nyeri kwa mpango wa kubuni kiwanda cha maparachichi, akieleza kwamba hatua hiyo itawainua kimapato.

Bi Agnes Njambi, mkulima Nyeri ameambia Taifa Leo mikakati ya serikali ya kaunti hiyo italeta afueni kwa wakulima wa maparachichi.

Baadhi ya wakulima eneo hilo wamekuwa waking’oa mikahawa na majani chai ili kupanda maparachichi, hasa ya hass.

Hass ni maparachichi yaliyoimarishwa kwa njia ya kupandikiza na yenye mazao ya kuridhisha.

Mkondo huo umeonekana kuigwa na kaunti ya Kericho, Nandi na hata Uasin Gishu, kupitia shinikizo la viongozi. Avocado za kupandikiza huchukua muda wa kati ya miaka mitatu hadi minne ili kuanza kuzalisha matunda baada ya upanzi.