Dondoo

Nyoka wavamia pasta akitimua mapepo

January 14th, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

Kasikeu, Makueni

Hali ya taharuki ilitanda eneo hili pasta mmoja msifika aliposhambuliwa na nyoka wawili alipokuwa akijaribu kufukuza mapepo katika boma la jirani ya muumini wa kanisa lake.

Ripoti za mtaa zinaarifu kuwa, pasta huyo alitimua mbio za kufa kupona huku akipiga kamsa, nao nyoka hao wakapotea kimiujiza, tena kwa njia ya ajabu sana!

Kulingana na mdokezi wetu, mwenye boma hilo alimwendea jirani yake aliyekuwa ameokoka na kumsihi amsaidie kwa vyovyote vile kuyatoa mapepo yaliyokuwa yakisumbua familia yake kila siku.

Aliahidi kumletea Mtumishi wa Mungu aliyekuwa gwiji wa kuyakomoa mapepo ya kila sampuli.

Inasemekana kwamba, muumini huyo alimuarifu pasta masaibu na madhila ya jirani yake na siku ya kufukuza mapepo ikapangwa. Mwenye boma alitakiwa atafute sadaka nono .

Siku ilipowadia, pasta alifika katika boma hilo huku akiwa ameezeka Biblia kwapani na akaitisha sadaka kwanza ili aanze ‘kazi’ yake bila wasiwasi wowote.

Alikabidhiwa Sh5000 na akaanza kuomba kwa ndimi huku akizunguka boma hilo.

Tunaarifiwa kwamba, wakati pasta alipokuwa nyuma ya nyumba ya mwenyeji wake, nyoka wawili walichomoka kama swara kutoka kusikojulikana na kumshambulia.

Hata hivyo, alinusurika kiajabu na akachana mbuga huku akipiga nduru kwa hofu.

Hata hivyo, nyoka hao walitoweka kimiujiza na kuwaacha wengi vinywa wazi huku mwenye boma akijifungia ndani ya nyummba akiogopa kushambuliwa na umati huo uliokuwa umejaa mori.

”Hiki ni kisa cha ajabu mno eneo hili,” mkazi mmoja alisikika akisema.