Habari Mseto

Nyongeza ya ada za NHIF yapingwa

November 19th, 2018 1 min read

Na ERIC MATARA

SHIRIKISHO la Watumizi wa Bidhaa nchini (COFEK) limepinga mipango ya serikali kupandisha ada za malipo ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) hadi asilimia mbili ya mapato.

Alhamisi iliyopita shirikisho hilo lilikosoa mpango huo wa serikali na kusema ni lazima huduma za shirika la NHIF ziboreshwe kabla ada zipandishwe.

“NHIF haijafanyiwa marekebisho yoyote. Afisa Mkuu Mtendaji hakuajiriwa kwa kufuata mfumo unaofaa. Uwajibikaji haujaboreshwa. Kwa kuzingatia jinsi hali ilivyo, haitakuwa busara kuongeza fedha zaidi kwa hazina hiyo,” akasema Katibu Mkuu wa COFEK, Bw Stephen Mutoro.

Afisa huyo alisema anashuku kuna nia mbaya katika uamuzi wa kupandisha ada za NHIF wakati ambapo Wakenya wanakumbwa na gharama kubwa ya maisha.

Shirikisho hilo sasa linataka serikali iweke kando mpango huo hadi mabadiliko ya usimamizi yafanywe katika NHIF na pia kuwe na mjadala utakaojumuisha wananchi kuuhusu.

COFEK iliongeza kuwa juhudi zozote za kulazimisha nyongeza hiyo ya ada zitapingwa mahakamani.

Bw Mutoro alisema miaka mitatu haijapita tangu ada zilipopandishwa ilhali watu wasiofahamu hali ngumu ambayo wananchi wanapitia, wanataka kuongeza tena ada.

Mwezi uliopita, Naibu Rais William Ruto alisema wananchi wanaopokea mishahara ya juu wataanza kutozwa ada zaidi kila mwezi kwa NHIF.

Kulingana na Bw Ruto, hatua hiyo itawezesha NHIF kuboresha utoaji huduma kwa wananchi wa mapato ya chini bila kuleta hasara kwa hazina hiyo.

Wengine ambao wamewahi kupinga mpango huo ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli, ambaye alisema ni jukumu la serikali kutimiza haki za kikatiba kwa wananchi kwa kuwatolea huduma za ubora wa hali ya juu za afya. Alionya pia kwamba Wakenya milioni 2.4 walioajiriwa hawana uwezo wa kubeba mzigo wa kugharamia afya bora kwa Wakenya milioni 43.

COTU ina jumla ya wanachama milioni 2.5 ambao ni wafanyakazi wanaotozwa ada za NHIF kila mwezi kwa msingi wa sheria za leba.