HabariSiasa

Nyoro amnyorosha Baba Yao

August 9th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

NDOTO ya Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu kurudi kazini imegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kuamuru asalie nyumbani hadi kesi inayomkabili ya ufisadi wa Sh51 milioni isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Ngenya Macharia (pichani juu) Alhamisi aliamuru majukumu yake yatekelezwe na naibu wake James Nyoro pamoja na mawaziri.

Bw Waititu alipoachiliwa kwa dhamana alisema angeweza kuendelea na kazi yake nje ya ofisi lakini sasa amepigwa breki hadi uamuzi kuhusu kesi yake utakapotolewa.

Gavana huya hata alifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wikendi iliyopita.

“Sitabadilisha masharti ya dhamana aliyoweka Hakimu Mkuu Lawrence Mugambi kwamba Bw Waititu asiende katika afisi ya gavana wa Kiambu wakati kesi ya ufisadi inayomkabili ikiendelea,” alisema Jaji Macharia.

Jaji alisema iwapo atakubaliwa kutekeleza majukumu ya ugavana kama alivyotaka, atawavuruga mashahidi kwenye kesi hiyo.

Lakini Jaji huyo alimruhusu Bw Waititu kurudi katika afisi hiyo kuchukua stakabadhi zake za kibinafsi, kwa masharti kuwa ataandamana na afisa wa polisi anayechunguza kesi hiyo, pamoja na afisa atakayeruhusiwa na afisa mkuu wa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC).

Jaji huyo alisema itakuwa ni fedheha kwa Bw Waititu kuendelea kuhudumu katika wadhifa wake wa gavana huku washtakiwa wenzake, ambao ni wafanyakazi wa kaunti hiyo, wakikaa nyumbani kusubiri uamuzi wa kesi hiyo ya kashfa ya jumla ya Sh 588 milioni.

“Katiba inamtaka Gavana Waititu na magavana wengine wote kujichukua kwa njia ambayo haitashusha hadhi ya ofisi yao,” alisema Jaji Macharia.

Aliongeza kuwa maafisa wakuu wa serikali na magavana wanapasa kuletea afisi zao heshima wala sio kuzidunisha.

Kutoka kulia: Mawakili wa Serikali Alexander Muteti, Faith Mwilah, Anne Partet na Wakiyo Mwamburi wacheka huku jaji akitoa hukumu Agosti 8, 2019. Picha/ Richard Munguti

Alisema Bw Waititu anadaiwa kupokea kwa njia ya ufisadi Sh51.2 milioni akijua zimetoka kwa Kaunti ya Kiambu. “Tendo hili sio la heshima kwa wakazi wa Kiambu,” akasema Jaji Macharia.

Mahakama hiyo pia ilikataa kubadilisha uamuzi wa jaji Mumbi Ngugi aliyesema Kifungu cha sheria za kupambana na ufisadi nambari 62(6) kinasema afisa mkuu serikali akishtakiwa asiende katika afisi aliyokuwa akihudumu hadi uamuzi wa kesi inayomkabili utolewe.

Mahakama ilisema kuwa maadili ya Bw Waititu yamepakwa tope na hivyo hafai kuendelea kutekeleza majukumu yake hadi ithibitishwe kuwa hana hatia ama ana makosa.

“Kesi inayombakili Waititu ni mbaya na maslahi ya umma yanamhitaji akae nje ya afisi,” alisema jaji huyo.

Mahakama pia ilikataa kupunguza dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu aliyopewa Bw Waititu.

Lakini Jaji Macharia alimpunguzia dhamana waziri wa ujenzi wa Kiambu, Luka Mwangi Wahinya hadi Sh2 milioni pesa taslimu.

Bw Wahinya anakabiliwa na shtaka la kuidhinisha malipo ya Sh588 milioni kwa kampuni ya ujenzi ya Testimony Enterprises Limited inayomilikiwa na Charles Chege na mkewe Beth Wangeci.

Pia mahakama ilimpunguza dhamana ya Sh15 milioni pesa tasilimu iliyopewa Chege hadi Sh4 milioni.

Lakini mahakama ilikataa kubatilisha dhamana ya Sh1 milioni iliyopewa wanachama wa kamati ya zabuni Zacharia Njenga Mbugua, Joyce Ngina Musyoka, Simon Kibocho Kang’ethe, Anslem Gachukia Wanjiku na Samuel Muigai Mugo,

Wakili Tom Ojienda alisema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumtaka Bw Waititu kukaa nyumbani.