Habari Mseto

Nyoro aomba ushirikiano kuiboresha Kiambu

October 11th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kufanya ushauri na wafanyabiashara wote wa Kiambu ili kuboresha hali ya uchumi katika kaunti hiyo.

Naibu Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema kaunti hiyo ni sharti iwe na msimamo na mwelekeo mpya ili wakazi wahudumiwe vilivyo.

Alisema kila mkazi wa Kiambu ataendesha biashara yake kwa uwazi bila kudhulumiwa na yeyote.

“Singetaka kuona wafanyabiashara wakinyanyaswa bali natamani kuona kila moja akiendesha shughuli zake kwa amani,” alisema Dkt Nyoro.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi mjini Thika baada ya kufanya kikao na washika dau wanaoendesha biashara kubwa mjini Thika.

Alitoa hakikisho kwamba vipande vyote vya ardhi ya umma iliyonyakuliwa inarejeshwa kwa umma.

“Hatuwezi tukakubali ardhi ya umma itumiwe visivyo na wanyakuzi. Kwa hivyo, ni lazima irudi kwa mwananchi ambaye ndiye mwenye uwezo na haki,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema ataendelea kutoa huduma zake kwa wananchi bila ubaguzi wowote.

Malalamiko

Aliwahakikishia ushirikiano wake nao huku akiwahimiza watoe malalamiko yao wakati wowote wananyanyaswa ama kwa njia hii au nyingine.

Alisema lengo lake kuu ni kuona ya kwamba kila mwananchi wa kawaida anapata nafasi yake ya kufanya biashara bila kuleta ubaguzi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema wataendelea kumuunga mkono ili kufanikisha juhudi zake za kutekeleza wajibu wake.

Walipendekeza kila mfanyabiashara apewe nafasi ya kufanya kazi yake bila kuhangaishwa kila mara na maafisa wa kaunti.

“Sisi wafanyabiashara tunataka tufanye kazi kwa ushirikiano wa karibu na wewe. Tukishirikiana bila shaka Kiambu itapiga hatua kibiashara,” alisema Bw Wanyoike.

Wafanyabiashara bao walikiri kuwa hapo awali kumekuwa na mivutano ya hapa na pale, lakini kwa sababu naibu gavana Dkt Nyoro amejitolea kufanya kikao nao, bila shaka matakwa yao yatatatuliwa.

“Sisi washikadau hatuna ubaya na yeyote bali lengo letu kuu ni kuona ya kwamba tunashirikiana pamoja na kushauriana kila mara,” alisema Bw Wanyoike.

Baadhi ya washikadau waliotoa maoni yao walipendekeza kuwe na vikao maalumu vya kila mara ili kuelewa mengi kuhusu yale yanayotendeka katika kaunti ya Kiambu.