Habari Mseto

Nyota Kaka alivyoachwa na mke kwa kuwa ‘mzuri kupindukia’

April 20th, 2024 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

CAROLINE Celico, ambaye ni mke wa zamani wa aliyekuwa mwanasoka matata wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Ricardo Izecson dos Santos maarufu Kaka, amefunguka kuhusu sababu ya ajabu iliyochochea kutemana kwao baada ya ndoa ya miaka 10.

Wapenzi hao wa tangu utotoni walifunga pingu za maisha 2005 na kuwa pamoja hadi walipotalikiana mwaka 2015. Ndoa yao ilijaliwa watoto wawili: mtoto wa kiume, Luca, 15, na binti, Isabella, 12.

Kulingana na gazeti la The Sun, Celico alisema kutengana kwao hakukuwa matokeo ya michepuko kwa sababu mumewe hakuwa kabisa na jicho la nje.

Kaka alikuwa mume mwaminifu aliyejali sana maslahi yake, kumtosheleza kikamilifu na kuwajibikia familia kwa upendo. Walakini, licha ya kuwa mume mzuri Celico kwa wakati fulani alihisi “utupu usioelezeka” katika ndoa na alikosa furaha.

“Kaka hakuwahi kunisaliti. Alinitendea mema, lakini sikuwa na furaha wakati mwingine. Kuna ‘kitu’ kilikosekana ambacho hadi leo sijui ni nini hasa! Nadhani pengine tatizo kuu ni alikuwa ‘mkamilifu’ na mzuri kupindukia,” Celico aliambia The Sun.

Kaka anajulikana kuwa mcha Mungu, na wakati wa ndoa yao Celico alijiunga na kanisa la mchezaji huyo mstaafu hata akawa mchungaji wa kiinjilisti.

Hata hivyo, mnamo 2010 aliacha kanisa na kuanzisha shirika la Horizontal Love lililoungana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali nchini Brazil kutoa misaada ya vyakula na rasilimali za elimu na usafi.

Baada ya kutemana na Celico, Kaka alipata penzi jipya kwa mwanamitindo mwingine raia wa Brazil, Carolina Dias, mnamo 2017.

Walichumbiana hadi Januari 2019 na wakafunga ndoa baadaye mwaka huo. Uhusiano wao umejaliwa binti mmoja anayeitwa Sarah.

Celico naye alianza kuchumbiana na mburudishaji na mjasiriamali Eduardo Scarpa Juliao mnamo 2016, mwaka mmoja baada ya kutengana na Kaka.

Walikula yamini ya ndoa 2021 katika sherehe ya kitamaduni iliyofanyika katika kanisa moja jijini Sao Paolo, Brazil. Wanatarajia mtoto wao wa kwanza.