MakalaMichezo

Nyota kwa Manchester United mastaa wapya waking’aa

Na LABAAN SHABAAN August 17th, 2024 2 min read

BAO la dakika ya lala salama yake mshambuliaji mpya wa Manchester United Joshua Zirkzee liliwapa Red Devils ushindi muhimu dhidi ya Fulham Ijumaa usiku.

Wachezaji wapya walianikwa ugani Old Trafford kutambulishwa kwa mashabiki, miongoni mwao akiwa mshindi wa mechi Zirkzee.

Mchezo ulikuwa kama wa pata potea kwa vijana wa nyumbani wa Erik ten Hag waliokuwa wanatafuta mtindo wa kuwakaba Fulham.

Ukosefu wa mtindo maalum wa kusakata kabumbu bado ulidhihirika kama ulivyoshuhudiwa msimu uliopita.

Kuna matumaini

Lakini mchambuzi wa kandanda Gary Neville amesema mashabiki wana matumaini ya kuona Manchester United mpya mwaka huu.

“Hawakuonekana kama wangeshinda mechi kwa sehemu kubwa ya mchezo. Ulinzi utakuwa bora zaidi ya msimu uliopita sababu kikosi kimekuwa kikubwa,” alisema Neville, akieleza kuwa United kukosa kufungwa bao katika mechi ya kwanza ilikuwa muhimu.

“Haukuwa mchezo wa kupendeza usiku huu lakini sikutarajia iwe hivyo ikizingatiwa walivyopanga kikosi. Sidhani tunaweza kuona timu thabiti ya Manchester United hadi kuwe na mfumo fulani.”

Sancho alienda wapi?

Katika kikosi cha United kumenyana na Fulham, Jadon Sancho hakuonekana.

Hii ni licha ya kushiriki mechi za maandalizi ya msimu katika ziara ya Amerika.

Erik ten Hag alithibitisha kuwa asingeshiriki kipute kwa sababu ya maumivu ya sikio.

“Ninaweza kuwa na wachezaji 20 tu. Jadon alikuwa na maambukizi sikioni juma hili kwa hivyo hakuwa katika kiwango cha asilimia 100. Angecheza lakini lazima ningefanya maamuzi,” alifunguka.

Zirkzee ang’aa

Ilimchukua Rasmus Hojland majaribio 15 kimiani kabla ya kufunga bao lake la kwanza kwa United.

Kwa hivyo Red Devils watafurahia baada ya Zirkzee kuanza kucheka na wavu upesi ugani Old Trafford.

Pengine matokeo haya ni ishara kuwa Mholanzi huyu anaweza kufana katika Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza.

Baada ya mchuano, Erik ten Hag alifichua kuwa, jinsi United ilifunga bao ni tokeo la mazoezi.

“Lazima tuwe naye (Joshua Zirkzee) ugani na lazima afike kwenye kisanduku. Tunamtaka aungane na kikosi ndiyo maana tulimnunua,” alieleza Meneja wa Man United.

Kazi kwa Ten Hag

Ili apate kikosi cha kumletea matokeo, Kocha wa United anatazamia kuleta mshikamano kikosini hasaa baada ya kuwasili kwa wachezaji wapya.

Noussair Mazraoui alishiriki mechi ya kwanza ya msimu siku chache baada ya kutua kutoka Bayern Munich.

Mazraoui alikuwa mchezaji mwenye pasi nyingi zaidi ya kwa asilimia 92 miongoni mwa wachezaji walioshiriki mchuano kati United na Fulham.

Nguvu mpya mwingine Matthijs De Ligt aliingia kwa nafasi ya Harry Maguire kama bado mechi ilikuwa sare.

Wachambuzi wa mchezo wanaamini hatimaye De Ligt atamwondoa Maguire kwenye ngome ya ulinzi.