Michezo

NYOTA PEKEE: Manchester City yafuta aibu ya Uingereza

September 20th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

HARKIV, Ukraine

MANCHESTER City iliondolea timu za Uingereza aibu ya kuanza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya vibaya baada ya kuponda miamba wa Ukraine Shakhtar Donetsk 3-0 katika mechi ya Kundi C, Jumatano.

City, ambayo ilipata pigo katika juhudi zake za kutetea taji la Ligi Kuu ya Uingereza ilipozimwa 3-2 na Norwich wikendi iliyopita, ilimalizia hasira yake kwa Donetsk kupitia mabao ya Riyad Mahrez, Ilkay Gundogan na Gabriel Jesus na kuwa klabu ya pekee kutoka Uingereza iliyoanza mechi za makundi kwa ushindi.

Iliingia uwanjani siku moja baada ya Chelsea kuchabangwa 1-0 na Valencia kutoka Uhispania uwanjani Stamford Bridge katika mechi ya Kundi H nayo Liverpool ikiwa imelazwa 2-0 na Napoli nchini Italia mnamo Jumanne.

Tottenham ilitupa uongozi wa mabao mawili katika sare ya 2-2 dhidi ya Olympiacos katika mechi ya Kundi B nchini Ugiriki mnamo Jumatano.

Baada ya kunyamazisha Donetsk, kocha wa City, Pep Guardiola alisisitiza kuwa hakuwa na tashwishi kuwa vijana wake wanaweza kukabiliana na tatizo kubwa la mabeki kuwa nje kutokana na majeraha.

Mhispania huyo alilazimika kutumia kiungo raia wa Brazil, Fernandinho kama beki wa kati baada ya Aymeric Laporte na John Stones kuingia mkekani majuzi.

Hata hivyo, Fernandinho alijaza nafasi hiyo vyema, huku City ikifurahia kuwa juu mabao 2-0 wakati wa mapumziko kupitia Mahrez na Gundogan uwanjani Metalist.

Jesus aliongeza bao la tatu katika dakika za lala-salama na kuhakikishia timu yake alama tatu muhimu ugenini.

“Mnaposhinda, kocha huwa amefanya maamuzi mazuri. Mnapopoteza, kocha huwa amefanya maamuzi mabaya. Tulipoteza mechi moja ndani ya miezi minane na hatutatilia shaka wachezaji hawa tulionao. Ninaonea fahari kuwa kocha wao,” alisema Guardiola.

“Tulilinda ngome yetu vyema na pia kujiundia nafasi za kupata mabao. Hatuna wachezaji wengi wa akiba katika safu ya ulinzi.

“Niko tu na Fernandinho. Yeye ni mchezaji mwerevu na stadi.

“Ana ujuzi mwingi na tabia na sifa za kipekee na anachosema wenzake hufuata. Yeye ni mchezaji muhimu sana kwetu.”

Fernandinho aliongeza, “Nimekuwa nikifanya mazoezi katika idara hiyo tangu msimu uanze. Pep anafahamu kila kitu kuhusu kikosi chetu na timu. Leo, nilipata fursa na natumai nitaweza kuimarika zaidi.”

Kocha atabasamu

Hata hivyo, Guardiola alikuwa na sababu ya kutabasamu kwa sababu beki Mfaransa Benjamin Mendy alishiriki mechi yake ya kwanza tangu mwezi Aprili baada ya kupona jeraha la goti. Aliingia uwanjani katika dakika za mwisho kama mchezaji wa akiba.

Huku Dinamo Zagreb na Atalanta wakikamilisha orodha ya washiriki kwenye kundi hili, City wanatarajiwa kutinga raundi ya 16-bora bila jasho.

Matokeo haya yalionyesha ukomavu katika kambi ya City, ambayo inalenga kushinda taji la Klabu Bingwa kwa mara ya kwanza kabisa.

City haijapita hatua ya robo-fainali ya Klabu Bingwa katika misimu mitatu iliyopita chini ya Guardiola. Mara ya mwisho ambapo Mhispania huyu alinyanyua taji hili ni mwaka 2011 akiwa Barcelona. Zagreb inaongoza kundi hili baada ya kupepeta Atalanta 4-0. Nambari mbili City itaalika Zagreb katika mechi yake ijayo.

Nayo Tottenham ilikalisha Mkenya Victor Wanyama kitini ikishuhudia mabao ya Harry Kane (penalti) na Lucas Moura yaliyopatikana dakika ya 26 na 30 mtawalia yakifuatwa na Daniel Poddence dakika ya 44 na Mathieu Valbuena aliyepachika penalti dakika ya 54.

Bayern, ambayo itazuru Tottenham katika mechi yake ijayo, iko juu ya jedwali baada ya kulima Red Star Belgrade 3-0 kupitia mabao ya Kingsley Coman, Robert Lewandowski na Thomas Muller.