Michezo

Nyota Sadio Mane avunja kimya baada kukemewa kuoa ‘mtoto’ mbichi

January 13th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

SADIO Mane, 31, hatimaye amevunja kimya baada ya kula yamini ya ndoa na mkewe Aisha Tamba mwenye umri wa miaka 18.

Nyota huyo wa zamani wa Liverpool alifunga pingu za maisha na tineja Aisha katika hafla ya kipekee siku chache baada ya kurejea Senegal kwa ajili ya Kombe la Afrika (AFCON), litakaloandaliwa nchini Ivory Coast kuanzia leo.

Akizungumza na vyombo vya habari wiki hii kufuatia harusi hiyo ya Jumapili iliyopita, Mane alishukuru kwa pongezi na zawadi tele kutoka kwa marafiki na wanasoka wenzake.

“Nimepongezwa na watu wengi, akiwemo rais wa nchi yangu ambaye amenitakia kila heri katika maisha ya ndoa,” alisema Mane kwa kufichua jinsi Rais wa Senegal, Macky Sall, alimtania wakati akipokea kikosi kitakachowakilisha Senegal AFCON.

“Alinipigia simu kunipongeza akasema ana zawadi yangu kisha akaomba Mungu aibariki nyumba yangu. Akaongeza kwamba kuanzia sasa nina kazi ya ziada ya kufanya; yaani kufunga mabao chumbani jinsi ninavyoyafunga ugani ” akaeleza.

Inasemekana jicho kali la fowadi huyo wa zamani wa Bayern Munich, ambaye sasa anasakatia Al Nassr ya Saudi Arabia, lilimuona Aisha kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita. Wala hakumkaribia rasmi wakati huo kwani umri halali wa msichana kuozwa nchini Senegal ni miaka 16.

Hata hivyo, Mane alimueleza mjomba wake – ambaye ni rafiki mkubwa wa babake Aisha – jinsi alivyotamani kidosho huyo awe wake wa halali.

Jarida la Pulse Sports nchini Senegal limedai kuwa Mane aligharimia karo yote ya Aisha akiwa mwanafunzi wa shule ya upili nchini Senegal.
Kwa mujibu wa gazeti la Sports Brief, uhusiano kati ya Mane na Aisha ulitakiwa kuwa wa siri.

Vile vile, harusi yao ilifaa kufanyika faraghani lakini marafiki, jamaa na wanasoka wenza walipopata fununu za mapema wakajitokeza kwa wingi kuhudhuria sherehe hiyo katika msikiti wa Keur Massar jijini Dakar.

Japo ripoti zingine zinadai umri kamili wa Aisha ni miaka 18, kuna tetesi kwamba ana miaka 26.

Hadi alipomtwaa Aisha kirasmi, Mane alikuwa ameweka siri maisha yake ya kimapenzi. Ni mara moja pekee – mnamo 2022- katika kipindi chote cha miaka sita alichokuwa kambini mwa Liverpool aliwahi kujadili masuala ya mapenzi hadharani akihojiwa na jarida la Tribune.

Alisema: “Nimeona wasichana wengi wakiuliza mbona sijaoa. Nimewaambia samahani, wanapoteza muda. Mke nitakayeoa hatakuwa kwenye mitandao ya kijamii. Natamani kuoa mwanamke msalihina na mcha Mungu. Hilo ndilo chaguo langu.”

Timu ya taifa ya Senegal ilitua Ivory Coast mnamo Jumanne usiku kwa ajili ya AFCON. Mabingwa hao watetezi wamepangwa katika kundi moja na Gambia, Cameroon na Guinea; wanapigiwa upatu kuhifadhi taji lao.

Kati ya picha za harusi zilizopakiwa na Mane kwenye Instagram, moja iliyotazamwa na zaidi ya watu laki moja chini ya saa 24 ilipigwa mbele ya bango kubwa lenye maandishi “Bw na Bi Mane”.