Nyota Shikangwa na Awuor watambulishwa rasmi Uturuki, Ufaransa

Nyota Shikangwa na Awuor watambulishwa rasmi Uturuki, Ufaransa

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI Jentrix Shikangwa Milimu na kipa Lilian Awuor wamezinduliwa rasmi na klabu zao mpya barani Ulaya.

Shikangwa alizinduliwa na Fatih Karagumruk SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kinadada nchini Uturuki naye Awuor ni mali ya Soyaux-Charente kutoka Ligi Kuu ya Kinadada nchini Ufaransa.

Awuor na Shikangwa walitokea klabu ya Vihiga Queens mnamo Januari 11 na Januari 21 mtawalia. Walishinda Ligi Kuu ya Kenya wakiwa Vihiga mwaka 2017, 2018 na 2019 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) 2021 iliyowapa fursa ya kujinadi zaidi Bara Ulaya kupitia kwa Klabu Bingwa Afrika nchini Misri baadaye mwaka huo.

Shikangwa, 20, amejiunga na Karagumruk kwa kandarasi ya mwaka mmoja naye Awuor,22, yuko Soyaux-Charente kwa mkataba wa miaka mitatu.

“Tumenyakua Milimu, winga mahiri wa timu ya taifa ya Kenya. Tunamtakia mafanikio anapoendeleza uchezaji wake hapa Karagumruk,” klabu hiyo ilisema kupitia mitandao yake kijamii.

Soyaux-Charente pia ilitangaza kumzindua Awuor kupitia mtandao ikisema ni mchezaji wa timu hiyo inayovalia jezi ya rangi ya samawati na nyeupe. Shikangwa na Awuor wote ni wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya maarufu kama Harambee Starlets.

You can share this post!

Everton wateua Frank Lampard kuwa kocha wao mpya

MWALIMU WA WIKI: Mwandishi stadi na mlezi wa vipaji

T L