NYOTA WA WIKI: Kylian Mbappe

NYOTA WA WIKI: Kylian Mbappe

Na GEOFFREY ANENE

KIGOGO Kylian Mbappe ni mchana-nyavu anayeaminiwa na Paris Saint-Germain na Ufaransa katika utafutaji wa mabao.

Wachanganuzi wa spoti na mashabiki wanaamini yumo mbioni kuwa mwanasoka bora siku moja kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Wana kila sababu ya kufanya hivyo kwa sababu kinda huyu mwenye umri wa miaka 22 tayari ameonyesha makubwa uwanjani.

Mbappe amechana nyavu mara 171 katika mechi 123 katika mashindano yote tangu aanze kutandaza soka ya watu wazima mwaka 2015 akiwa AS Monaco.

Kambini mwa Paris Saint-Germain, Mbappe amefikisha magoli 141 kutokana na michuano 101.

Mshambuliaji huyu, ambaye Wafaransa wenzake Antoine Griezmann na Presnel Kimpembe wamembatiza jina la utani Kiki na Donatello mtawalia, alianza kukuzwa kuwa mchezaji wa soka 2004.

Baba yake Wilfried Mbappe ndiye alikuwa fundi wake wa kwanza. Wilfried alikuwa kocha wa timu ya watoto ya AS Bondy.

Mbappe alipata pia kupitia mikononi mwa Rennes, Chelsea na Real Madrid, ingawa kwa kipindi kidogo sana.

Alilelewa zaidi na kituo cha kitaifa cha kukuza talanta nchini Ufaransa cha Clairefontaine. Alipiga hatua zake kubwa katika soka kambini mwa Monaco.

Mbappe, ambaye akiwa mdogo alienzi mshambuliaji matata Ronaldo, alikuwa kambini Monaco kwa miaka mitano kuanzia Julai 2013.

Aliwahi kualikwa na Chelsea, Madrid, Liverpool, Manchester City na Bayern Munich kufanyiwa majaribio.

Mshambuliaji huyu anayeweza kutumika pembeni kushoto na kulia, mshambuliaji mkuu na pia kama kiungo mshambuliaji, aliingia timu ya watu wazima ya Monaco kwa mara ya kwanza mwaka 2015.

Alikuwa muhimu katika Monaco kupiku miamba PSG katika vita vya kutwaa taji la Ligue 1 msimu 2016-2017 alipochangia mabao 26.

Yeye ndiye tineja ghali katika historia ya soka baada ya PSG kumnunua kwa karibu Sh23.0 bilioni kutokea Monaco.

Msimu huu pekee, Mbappe ametikisa nyavu mara saba na kumega idadi sawa ya pasi – asisti – zilizozalisha magoli katika michuano 15 ya Ligue 1.

Pia, ana mabao mawili na asisti tano katika mechi tano za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kimataifa, Mbappe ameifungia magoli 24 na kusuka pasi 20 zilizozalisha mabao katika mechi 53 tangu Machi 25 mwaka 2017 alipoanza kuchezea Les Bleus.

Mbappe ni mfungaji bora wa Ligue 1 misimu mitatu (2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021).

Mchango wake kwenye soka umeshuhudia akijumuishwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora duniani (Ballon d’Or) mara nne.

Alikamata nafasi ya saba mwaka 2017, nambari nne mwaka 2018, nambari sita mwaka 2019 na nambari tisa mwaka 2021.

Kifedha, Mbappe ni mmoja wa wanasoka wanaovuna vinono katika mchezo huu.

Kambini mwa PSG, Mbappe anaaminika kupokea Sh60.3 milioni kila wiki.

Yuko nyuma ya masupastaa wenzake Neymar (Sh128.6 milioni) na Lionel Messi (Sh74.9 milioni).

You can share this post!

Kenya yaendea Morocco fainali ya kufa-kupona kuingia Kombe...

DIMBA: Harusi tunayo! Ya Trapp na Izabel

T L